Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Arusha
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza katika miaka mitano ijayo Serikali imejipanga kuboresha miundombinu mbalimbali ya mji wa Arusha ikiwemo masoko ya kisasa na barabara za lami.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha leo Oktoba 2,2025 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ,Dk.Samia amesema kwa muda mrefu jiji hilo la Arusha lilikuwa halina stendi ya sasa lakini sasa tayari ujenzi umeanza takribani sh. bilioni 14.3 zinatumika katika mradi huo uliopo Bondeni City.
Pia, amesema katika eneo hilo la Bonden City Serikali inakwenda kujenga soko kubwa la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga.
“Katika kipindi cha miaka mitano tumejenga soko la Mbauda kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo. Vilevile tutaendelea na ujenzi wa masoko mawili mengine eneo la Morombo na Kilombero kwa thamani ya Sh.bilioni 30.6.”
Pia amesema Kwa Arusha amesema tayari vikundi 853 vya wajasiriamali vimenufauka na zaidi ya Sh.bilioni 10.4 zimetumika huku serikali ikijipanga kuanzisha mfuko maalum kwa wafanyabiashara ndogondogo.
Kuhusu mahitaji ya maboresho ya barabara za ndani ya Jiji la Arusha ambapo jiji hilo limejumuishwa katika mradi wa TACTIC ambapo jumla ya kilometa 10.2 zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Baadhi ya barabara hizo ni Oljoro kilometa 4.7, Engosheraton kilometa 4.8, Olasiti kilometa 4 ambazo zitajengwa ili Jiji la Arusha lipate hadhi yake ya kuwa jiji hasa ukizngatia watalii zaidi wanafika katika jiji hilo.“Reli za kisasa zitakuja hivyo lazima jiji hilo liwe na mtandao wa barabara za lami.”