NOTTINGHAM: MENEJA wa Nottingham Forest, Ange Postecoglou, amesema hakushtushwa na mashabiki wa klabu hiyo kutaka afukuzwe kazi baada ya kipigo cha 3-2 kutoka kwa Midtjylland kwenye Europa League usiku wa Alhamisi huku akisema analenga zaidi kuboresha kikosi hicho na kupata matokeo chanya.
Postecoglou, ambaye aliteuliwa mwezi uliopita kuchukua nafasi ya Nuno Espirito Santo, hajapata ushindi wowote katika michezo sita ya kwanza akiwa kocha wa Forest. Hiyo imemfanya kuwa meneja wa kwanza wa kudumu wa klabu hiyo katika kipindi cha miaka 100 kushindwa kupata ushindi katika mechi yoyote kati ya sita za kwanza kazini.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 60 na aliyewahi kuinoa Tottenham Hotspur, alisikika akishutumiwa na mashabiki waliopiga kelele: “Unafukuzwa asubuhi” baada ya kipigo hicho kwenye Uwanja wa City Ground. Postecoglou amesema anaelewa hasira zao.
“Wanaruhusiwa kuwa na maoni yao. Nilisikia kilio chao, Hakuna kinachonishtua kwenye soka. Hivyo ndivyo hali ilivyo. Wajibu wangu ni kuhakikisha tunapata ushindi na kuendeleza timu hii. Naweza kubadilisha mtazamo wa watu kwa kushinda mechi.” – alisema kocha huyo.
“Ninafahamu hali ya sasa haipendezi na mtazamo wa wengi ni hasi, hasa kuelekea kwangu, Lakini si jambo geni kwangu. Naamini bado tupo kwenye njia sahihi.” – aliongeza Postecoglou.
Forest kwa sasa wapo nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwa na pointi tano pekee kutoka kwenye mechi sita. Ratiba yao ya Oktoba haionekani kuwa rahisi, ikiwasafirisha hadi ugenini dhidi ya Newcastle United Jumapili, kisha nyumbani na Chelsea kabla ya safari nyingine ya Bournemouth.
The post “Kelele za mashabiki hazinishtui” – Postecoglou first appeared on SpotiLEO.