LIVERPOOL: KIPA wa Liverpool, Alisson Becker, atakosa michezo kadhaa ya kirafiki ya timu ya Taifa ya Brazil baada ya kupata jeraha la misuli ya paja katika mchezo wa Katikati ya wiki wa ligi ya mabingwa ulaya, na huenda pia akakosa mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester United baada ya mapumziko ya kimataifa.
Alisson alipata jeraha hilo wakati wa kipindi cha pili cha kipigo cha 1-0 dhidi ya Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa, Jumanne usiku, alipojaribu kuokoa mpira akiwa anarudi nyuma kuelekea langoni mwake.
Meneja wa Liverpool, Arne Slot, tayari amethibitisha kuwa kipa huyo hatakuwepo kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Chelsea. Aidha, amethibitisha kuwa Alisson hatajumuishwa kwenye kikosi cha Brazil kitakachocheza mechi za kirafiki dhidi ya Korea Kusini Oktoba 10 na Japan Oktoba 14.
Kuhusu muda wa kurejea kwake, Slot amesema: “Inategemea kasi ya kupona kwake. Ni wazi hatacheza Jumamosi, hataichezea Brazil, na itakuwa ajabu kama atakuwa tayari kwa mchezo wa kwanza baada ya mapumziko ya kimataifa dhidi ya Manchester United, Oktoba 19, pale Anfield. Kuanzia hapo, mambo yanaweza kwenda haraka au kuchukua muda zaidi. Ni vigumu kutabiri.”
Kutokuwepo kwa Alisson kunampa nafasi mchezaji mpya, Giorgi Mamardashvili wa Georgia, aliyejiunga kutoka Valencia, kuweka mizizi golini hapo kama kipa wa kwanza wa Liverpool katika kipindi hiki kigumu.
The post Kipa Liverpool kuikosa Chelsea, United first appeared on SpotiLEO.