DAR ES SALAAM: TIMU ya taifa ya Tanzania ‘taifa stars’ inatarajia kuingia kambini kesho kujiandaa na michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Zambia na Iran.
Mchezo wa kwanza ni wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia utakaochezwa Zanzibar Oktoba 8, mwaka huu.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Clifford Ndimbo amesema kikosi kitakaa kambi ya siku mbili Dar es Salaam kisha kitaenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza.
“Mchezo utachezwa Oktoba 8 saa 4:00 usiku. Licha ya kutofuzu bado ni mchezo muhimu, tunahitaji pointi nyingi kumaliza hatua ya makundi katika historia,”alisema
Ndimbo alisema: “Tunauendea mchezo kwa umuhimu mkubwa kuhakikisha tunafanya vizuri. Baada ya mchezo dhidi ya Zambia kikosi kitakaa siku mbili kisha kitaenda Dubai kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Iran,”
Mchezo dhidi ya Iran utachezwa Oktoba 14, mwaka huu Dubai ambapo amesema wanataka kutumia kujipima na moja ya taifa ambalo lina ubora wa viwango vya juu.
“Iran ni moja ya mataifa 21 yenye viwango vya juu vya soka. Ni jambo kubwa kwetu na tunauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa,”alisema.
The post Taifa Stars yaiendea Zambia, Iran Kambini first appeared on SpotiLEO.