Mkurugenzi idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akielezea umuhimu wa huduma za dharura wakati wa mafunzo ya siku nne kwa wataalamu wa afya ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa na Shirika la Cardio Star International la nchini Marekani katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Rais wa Shirika la Cardio Star International la nchini Marekani Dkt. Miroslav Peev akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa wataalamu wa afya ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Shirika la Cardio Star International la nchini Marekani Dkt. Richard Harper akiwafundisha wataalamu wa afya jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura wakati wa mafunzo hayo ya siku nne yanayotolewa na Shirika hilo katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa usingizi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Faraji Lydenge akichangia mada wakati wa mafunzo ya siku nne ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa na Shirika la Cardio Star International la nchini Marekani yaliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Watalaamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini wakifuatilia mada zilizokuwa zikiendelea wakati wa mafunzo ya siku nne ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa na Shirika la Cardio Star International la nchini Marekani katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na: JKCI
………..
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Saalam.
Wataalamu wa afya 115 kutoka hospitali mbalimbali nchini wameshiriki katika mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani.
Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam ambapo wataalamu kutoka Hospitali ya Bugando Medical Center (BMC), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Mwananyamala (MRRH), na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) wameshiriki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watalaamu wanaotoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi ili waweze kutoa huduma kwa viwango vya juu na kuokoa maisha yao.
“Tumekuwa tukishirikiana na Shirika hili la Cardio Start International ili kwapamoja tuendelee kuwajengea uwezo wataalamu wetu nchini na kuboresha huduma za dharura katika nchi yetu” alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Rais wa Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani Dkt. Miroslav Peev alisema mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu wa afya wanaotoa huduma za dharura kuongeza ujuzi katika kutekeleza majukumu yao.
“Ni matumaini yangu kupitia mafunzo haya tutajifunza kwa pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya mambo muhimu ya kuzingatia pale tunapotakiwa kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka”, alisema Dkt. Mirolsav.
Wakizungumzia mafunzo hayo washiriki kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyama (MRRH) na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) walisema mafunzo hayo yanawasaidia kutambua mapema wagonjwa wa dharura na wenye matatizo ya moyo ili waweze kuwasaidia kwa wakati.
“Kupitia mafunzo haya tutaweza kutoa maamuzi ya haraka kama mgonjwa anatakiwa kupewa rufaa ama tunaweza kumuhudumiwa katika hospitali yetu kwasababu kazi yetu ni kuokoa maisha ya watu”, alisema Hans John kutoka Hospitali ya mwananyamala.
“Katika mafunzo haya nina matarajio mengi ukizingatia siku hizi teknolojia imeongezeka hivyo kupitia mafunzo haya naamini tutaenda kuboresha huduma tunazozitoa”, alisema Paul Byalugaba kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH).