

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake mkoani Manyara Oktoba 4, 2025, ambapo amehutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Babati mjini.
Akizungumza katika mkutano huo uliopambwa na shamrashamra za wafuasi wa CCM, Dkt. Samia amewataka wananchi wa Manyara kuendelea kuiamini CCM, akisema chama hicho ndicho chenye rekodi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
“CCM tumetekeleza miradi mikubwa ya maji, umeme, elimu, afya na miundombinu. Tumejenga barabara, tumeimarisha huduma za jamii na tutaendelea kufanya zaidi kwa ajili ya Watanzania wote bila ubaguzi,” amesema Dkt. Samia huku akishangiliwa na wananchi.
Ameongeza kuwa serikali itazidi kuwekeza katika kuinua sekta ya kilimo, hususan kwa wakulima wa Manyara, ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia pia amewasihi wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano wakati huu wa kampeni, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi moja inayopaswa kuweka mbele maslahi ya kitaifa.
“Amani ndiyo nguzo ya maendeleo. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa au kikanda. CCM itabaki kuwa chama cha umoja na maendeleo,” amesisitiza Dkt. Samia.
Mkutano huo ni sehemu ya muendelezo wa kampeni za CCM ambapo Dkt. Samia amekuwa akipita mikoa mbalimbali nchini kusaka ridhaa ya wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.