
Chake Chake, Kusini Pemba – Oktoba 6, 2025
Mke wa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mama Mariam Mwinyi, ametoa wito kwa wanawake wa Kisiwa cha Pemba kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha Dkt. Hussein Ali Mwinyi anapata kura za kutosha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili aendelee kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio zaidi.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa wanawake ulioandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) na kufanyika katika Uwanja wa Kufurahishia Watoto Tibirizi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba leo tarehe 06 Oktoba 2025.
Aidha, Mama Mariam amewahimiza wanawake kusimama imara nyuma ya Dkt. Mwinyi, akisisitiza kuwa kura za wanawake zina nafasi kubwa katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya Zanzibar.
Mariam Mwinyi amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi, Serikali ya Awamu ya Nane imefanikiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025 kwa mafanikio makubwa, hususan katika sekta za elimu, afya, uwezeshaji wanawake, na miundombinu.
“Wanawake mmeshuhudia wenyewe jinsi Serikali ya CCM ilivyojitoa kuwahudumia kwa vitendo. Hii ni sababu tosha ya kuhakikisha tunamlinda na kumuunga mkono Dkt. Hussein Mwinyi ili aendelee kutuletea maendeleo zaidi,”
— amesema Mama Mariam Mwinyi.
Halikadhalika, Mariam Mwinyi amewataka wanawake wa Pemba kuwa mabalozi wa amani, umoja na mshikamano, huku wakihamasisha wenzao kushiriki uchaguzi kwa amani na kumpigia kura Mgombea wa CCM, ili chama hicho kiendelee kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa.