Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Ezekiel akizungumza jambo na Mzee Maulid Ngakonda ambaye ni Mlemavu wa miguu, mkazi wa Kata ya Toangoma, Mtaa wa Kongowe – Mzinga A, wakati Wafanyakazi wa Mkoa huo walipomtembelea nyumbani kwake leo Oktoba 7, 2025, Dar es Salaam na kufanikiwa kumfanyia kazi ya uwekaji wa mtandao wa umeme ndani ya nyumba yake pamoja na kumunganisha nishati ya umeme bila gharama yoyote ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
…………….
Katika muendelezo wa kuadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, limechukua hatua ya kumsaidia Mzee Maulid Ngakonda ambaye ni Mlemavu wa miguu, mkazi wa Kata ya Toangoma, Mtaa wa Kongowe – Mzinga A, kwa kumfanyia kazi ya uwekaji wa mtandao wa umeme ndani ya nyumba yake pamoja na kumunganisha nishati ya umeme bila gharama yoyote.
Msaada huo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii, hasa kwa watu wanaokabiliwa na changamoto za maisha, sambamba na kuunga mkono makundi yenye uhitaji maalum, katika kipindi hiki cha kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja.
Akizungumza leo 7 Oktoba 2025 jijini Dar es Salaam, baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Ezekiel Mashola ameeleza kuwa uamuzi huo umetokana na ombi lililowasilishwa na Mzee Ngakonda, ambaye alifika ofisi za TANESCO Wilaya ya Mbagala akiwa na uhitaji wa huduma ya umeme, akiwa hana fedha.
“Katika kuadhimisha siku ya pili ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, tumechukua jukumu la kumfanyia wiring nyumbani kwake. Zaidi ya hilo, tutamkabidhi jiko janja linalotumia umeme kidogo ili kumsaidia kuachana na matumizi ya nishati chafu” amesema Mhandisi Mashola.
Kwa upande wake, Mzee Ngakonda ameushukuru uongozi TANESCO kwa msaada huo, huku akieleza kuwa umeme huo utabadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa, hasa ikizingatiwa kwa muda mrefu alikuwa akitumia vyanzo visivyo salama vya kupata mwanga, ambavyo vimesababisha matatizo ya kiafya kutokana na moshi.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzinga A, Bw. Lucas Kavindi ametoa pongezi kwa TANESCO Mkoa wa Temeke kwa hatua hiyo, ambapo ameeleza kuwa jambo hilo ni la kipekee kwa taasisi kumfikia mwananchi mwenye changamoto kubwa ya maisha.
“Tunaona kazi nzuri inayofanywa na TANESCO Temeke, kuwafikia watu wasio na uwezo kama Mzee Ngakonda ni jambo la kuigwa. Ni tukio la kwanza kushuhudia huduma ya namna hii katika mtaa wangu,” amesema Bw. Kavindi.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kimataifa kila mwaka katika wiki ya kwanza ya Oktoba, ikiwa ni jukwaa kwa mashirika kuonyesha kuwathamini wateja wao kupitia utoaji wa huduma zenye ubora, kusikiliza mrejesho na kutatua matatizo.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Mpango Umewezekana.”