DAR ES SALAAM:KUELEKEA mchezo wao muhimu wa Kombe la Shirikisho Afrika, klabu ya Azam FC imerejea katika mazoezi makali huku ikitamba kuwa iko tayari kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania dhidi ya KMKM ya Zanzibar, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Spotileo Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe, alisema maandalizi ya timu hiyo yanaendelea vizuri licha ya kuwepo kwa baadhi ya wachezaji ambao wanakosekana kwa sababu mbalimbali.
“Ni mechi ngumu sana kwa sababu kila timu inatafuta namna ya kuifanya nchi yake ijivunie. Lakini sisi tunaamini kuwa timu yoyote itakayovuka kati ya KMKM na Azam FC, basi Tanzania ndio itakayokuwa imevuka,” alisema Ibwe.
Aliongeza kuwa maandalizi ya mchezo huo ni sehemu ya dhamira ya klabu hiyo ya kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na heshima katika mashindano ya kimataifa.
“Tunaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika. Kama viongozi tumejiandaa. Ni kiu ya mashabiki kuona tunafanya vizuri, na sisi tunapambana kuhakikisha tunafanikisha hilo,” aliongeza.
Ibwe alisema kuwa mchezo huo si tu wa klabu, bali ni wa taifa zima kwani Azam FC inabeba matumaini ya Watanzania katika ngazi ya kimataifa.
Kwa sasa, kikosi cha Azam FC kipo kambini kikiendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa KMKM katika mchezo huo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo matokeo ya jumla yatatoa mwakilishi mmoja wa Tanzania katika hatua inayofuata.
The post Azam FC yajipanga dhidi ya KMKM first appeared on SpotiLEO.