DAR ES SALAAM:PAMBANO la ngumi la Knockout ya Mama msimu wa sita linatarajiwa kupigwa kesho Dar es Salaam likiwakutanisha mabondia 14 kutoka mataifa mbalimbali.
Tukio hilo, linaloandaliwa na Mafia Boxing Promotion, limepewa jina la kimataifa la “Usiku wa Vitasa – Ngumi Jiwe”, na linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya ngumi nchini mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amethibitisha kuwa tukio hilo linaungwa mkono rasmi na Serikali, huku Rais Dk Samia Suluhu Hassan akiahidi zawadi nono kwa mabondia watakaofanya vizuri.
“Mhe. Rais atatoa shilingi milioni 10 kwa bondia atakayeshinda kwa Knockout na milioni 5 kwa atakayeshinda kwa pointi katika pambano la mkanda wa kimataifa,” alisema Msigwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari Oktoba 9, jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inatilia mkazo maendeleo ya michezo kama sekta muhimu ya ajira, afya na heshima ya taifa.
“Ni tukio linalopendwa sana na mashabiki, na linaendelea kuinua mabondia wetu kifikra na kimataifa. Kwa kweli ni fahari kwa Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Mafia Boxing Promotion, maandalizi yamekamilika, na mashabiki wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani hiyo ya hali ya juu.
Mabondia watakaochuana ni Kalolo Amiri (Tanzania) vs Brama Krishnan (India), Yusuf Changarawe (Tanzania) vs Keneth Lukyamuzi (Uganda), Idd Pialari (Tanzania) vs Ronald Miro (Uganda), Mchanja Yohana (Tanzania) vs Aldri Portillo (Venezuela), Ibrahim Mafia (Tanzania) vs Alvin Camique (Philippines), Salmin Kassim (Tanzania) vs Canny Kotey (Ghana) na Juma Choki (Tanzania) vs Manikandan V (India)
The post Ngumi za kimataifa kutesa Dar kesho first appeared on SpotiLEO.