CASABLANCA:TIMU ya taifa ya Misri (Pharaohs) imefuzu rasmi kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Kanada na Mexico, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Djibouti, na kujihakikishia nafasi ya kwanza kwenye Kundi A ikiwa na mechi moja mkononi.
Furaha hiyo inarejesha matumaini ya soka la Misri baada ya kukosa kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2022 huko Qatar.
Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Pharaohs kushiriki fainali hizo, baada ya kushiriki awali mwaka 1934, 1990 na 2018.
Misri imekuwa kwenye kiwango bora kipindi chote cha kufuzu, chini ya kocha mkuu Hossam Hassan, ambaye ameunganisha nidhamu ya kiulinzi na mashambulizi ya kasi.
Katika michezo tisa ya kufuzu, Misri imefunga mabao 19 huku ikiruhusu mabao mawili tu, na imeweka ‘clean sheet’ saba (bila kufungwa bao).
Mlinzi mkongwe Mohamed El Shenawy, ambaye pia anaibuka na umahiri mkubwa katika mashindano ya FIFA Club World Cup 2025 akiwa na Al Ahly, ameendelea kuwa ngome muhimu golini.
Nahodha wa timu, Mohamed Salah, ameonesha kiwango cha juu kwa kufunga mabao tisa, akifuatwa na Mahmoud Trezeguet aliyechangia mabao matano, huku Ahmed Sayed ‘Zizo’ akifunga mabao mawili.
Wachezaji wazoefu kama Salah na Trezeguet, waliokuwemo katika kikosi cha 2018, wameungana na nyota wachanga kama Omar Marmoush na Mostafa Mohamed, ambao wanaongeza kasi na makali katika safu ya ushambuliaji.
Katika ulinzi, beki Mohamed Abdelmonem anayekipiga kwenye klabu ya Nice ya Ufaransa, ameonesha uimara mkubwa sambamba na El Shenawy.
Licha ya kushiriki Kombe la Dunia mara tatu zilizopita, Misri haijawahi kushinda mchezo wowote katika fainali hizo wala kuvuka hatua ya makundi.
The post Salah aiongoza Misri kufuzu Kombe la Dunia 2026 first appeared on SpotiLEO.