Na Meleka Kulwa- Dodoma
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB0, imelaani vikali tukio la taarifa za kushambuliwa na kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Humphrey Pole Pole linalodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana tarehe 06 Oktoba, 2025 majira ya saa 08:30 usiku katika eneo la Ununio Jijini Dar es salaam alipokuwa anaishi ambalo limeleta taharuki kwenye jamii.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu kwenye taarifa aliyoitoa juu ya kulaani vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora hukua akiongeza kuwa katika ufuatiliaji wake THBUB imebaini vitendo hivo vimeambatana na ukatili dhidi ya ubinadamu.
“THBUB inalaani na kukemea vikali vitendo hivyo kwani matukio kama haya ni uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ambayo yanahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu,”amesema.
Katika taarifa yake Mhe. Mwaimu ameongeza kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoeleza kuwa kila mtu anayohaki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria na kwamba kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.
“Hivyo THBUB inalaani vikali vitendo hivyo, ukatili dhidi ya binadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoeleza kuwa ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha,”amesema.
Pia, ameongeza kuwa THBUB inatambua jitihada na maelekezo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali, viongozi wa dini pamoja na Jeshi la Polisi kukemea matukio hayo nchini hivyo, inapendekeza Jeshi la Polisi Tanzania liwatafute na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika na matukio hayo ambayo yanaenda kinyume na misingi ya haki za binadamu na utu.
“Lichukue hatua mahsusi kuimarisha ulinzi katika maeneo ya wananchi na kuwezesha kupata taarifa za mapema kuhusu kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa sheria ikiwa ni pamoja na mauaji na vitendo vya uvunjifu wa amani, kabla na baada ya matukio hayo kutokea kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo husika ili kusaidia ulinzi na usalama wa raia na mali zao,”ameongeza.
Amesema THBUB itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote katika jitihada za kukomesha matukio ya uvunjifu wa amani kwa kuelimisha umma kuhu haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kushauri njia muafaka za kuimarisha amani na utulivu katika nchi.