Na Meleka Kulwa- Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Bw. Juma Mkomi, amesema Serikali imetenga jumla ya nafasi mpya za ajira 41,500 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, zikiwemo nafasi 12,176 za walimu, Afya (Mamlaka za Serikali za Mtaa) nafasi 10,280, Wizara ya Kilimo nafasi 470, Wizara ya Mifugo nafasi 312, Wizara ya Uvuvi nafasi 47, ulinzi unaohusisha Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji 7,000 na Kada nyinginezo nafasi 11,022
Akizungumza Oktoba 11, 2025, jijini Dodoma kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara na waandishi wa habari, Bw. Juma Mkomi amesema kuwa utekelezaji wa ajira hizo unaanza mara moja, huku Sekretarieti ya Ajira ikiendelea kukamilisha mchakato wa ajira za mwaka wa fedha uliopita (2024/2025).
“Ninaielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza mchakato wa kujaza nafasi hizo za mwaka 2025/2026, pamoja na kukamilisha nafasi zote zilizobaki za mwaka uliopita,” amesema Bw. Mkomi.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitenga ajira 45,000, na hadi sasa nafasi 30,863 tayari zimeajiriwa na wahusika kupangiwa vituo vya kazi, 6,701 zipo katika hatua ya kupangiwa vituo, na 7,836 zinatarajiwa kukamilika kufikia mwezi Novemba 2025.
Aidha, Bw. Mkomi Amesema kuwa Sekretarieti ya Ajira imepewa mamlaka ya kusimamia ajira zote katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na waajiri mbalimbali, ikiwemo TAMISEMI, Ofisi ya Msajili wa Hazina, na Wizara ya Afya, ili kuhakikisha nafasi zote zilizotengwa zinajazwa kwa wakati.
“Waajiri wote wanapaswa kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya Ajira kuhakikisha zoezi la usaili linafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni,”amesema Bw. Mkomi
Akibainisha kuwa kwa mwaka huu, zoezi la usaili litafanyika katika kila mkoa wa Tanzania Bara na vituo maalum vya Zanzibar, ili kupunguza gharama kwa waombaji na kurahisisha ushiriki wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali,
Pia, amesema kuwa barua za ajira zitawasilishwa kupitia akaunti za Ajira portal. Hatutaki waombaji waje Dodoma kwa ajili ya kufuata barua” amesema Bw. Mkomi
“Waombaji watakaofaulu usaili lakini wakashindwa kupangiwa kazi mara moja watahifadhiwa kwenye kanzidata ili wapangiwe kazi kadri nafasi mpya zitakavyojitokeza,” Amesema Bw. Mkomi.
Pia, Bw. Mkomi amesema kuwa Serikali inaendelea kupunguza pengo la watumishi lililopo kwenye sekta mbalimbali, ambapo tathmini ya ofisi yake imebaini upungufu wa takribani zaidi ya watumishi 270,000. Hata hivyo, amepongeza jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutimiza ahadi ya kutoa ajira kila mwaka.
Aidha, Bw. Mkomi amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa usimamizi wa utendaji kazi wa watumishi wa umma kupitia mfumo wa kielektroniki wa (PEPMIS/PIPMIS). ili kuhakikisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi unaimarika.
“Ofisi itaendelea kuhakikisha mifumo ya kielektroniki inatumika kusimamia ajira, utendaji kazi na rasilimali watu ili kujenga utamaduni wa kuwajibika kwa hiari na kuongeza tija katika sekta ya umma,” amesema Bw.Mkomi
Pia, amewataka watumishi wa umma kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyooneshwa katika Wiki ya Huduma kwa Wateja, akisema kuwa ni chachu ya mabadiliko ya kiutendaji na kujenga taswira chanya ya Serikali.