Katika kuelekea kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Afya Club imeanza shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo maandamano, usafi wa mazingira na upimaji wa afya bure kwa wananchi wa Manispaa ya Songea.
Shughuli hizo zimeanza leo Oktoba 13 kwa maandamano kutoka ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Songea hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa ajili ya kufanya usafi, na baadaye kuelekea Soko Kuu la Songea ambako waliendelea na usafi pamoja na kutoa huduma ya upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Louis Chomboko alisema mkoa wa Ruvuma haukubaki nyuma katika kuenzi falsafa ya Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha usafi wa mazingira na upimaji wa afya unafanyika kwa wananchi wote bila malipo.
Amesema Mtu ni afya na afya ni mazingira. Zoezi la upimaji afya ni bure kuanzia leo hadi kesho. Uchafu wa mazingira unaweza kusababisha magonjwa ya ngozi, kuhara, na kutapika, hivyo kudumisha usafi kunaweza kuzuia magonjwa hayo.
Aliongeza kuwa falsafa ya Mwalimu Nyerere ya “Mtu ni Afya” inalenga kuimarisha afya ya jamii na kuchangia maendeleo ya taifa, na kwamba wananchi wanapata fursa ya kupima magonjwa kama kisukari na hali ya lishe.
Maadhimisho hayo pia yameambatana na hamasa ya kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, ambapo wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi bila kujali itikadi za vyama.
Asumta Kipanga, mmoja wa washiriki wa usafi, alisema kuwa wamejipanga kuendelea na shughuli hizo kwa heshima ya Baba wa Taifa na kuwataka vijana wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu kama sehemu ya kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankoo, aliwashukuru wananchi na watumishi wa umma waliojitokeza kushiriki usafi katika soko kuu na hospitali ya mkoa akisema tukio hilo liwe chachu ya kudumisha usafi katika maeneo yote ya umma na makazi.
Aidha, alisema kuwa maadhimisho ya kitaifa ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka huu yatafanyika mkoani Mbeya na yataenda sambamba na uzimaji wa Mwenge wa Uhuru, akibainisha kuwa falsafa ya “Uhuru na Kazi” itaendelea kuenziwa kama alama ya maendeleo ya taifa.