

Msanii wa muziki na maigizo, Agness Suleiman Kahamba, maarufu kama Aggybaby, ameshinda Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike wa Mwaka 2025 kutoka Achievers Awards International ya nchini Nigeria, kutokana na mchango wake mkubwa katika sanaa ya uigizaji na shughuli za kijamii kupitia taasisi yake ya Tupaze Sauti Foundation (Tanzania).
Waandaaji wa tuzo hizo wametambua ubora wa kazi za Agness katika sekta ya filamu, hususan kupitia tamthiliya “Panguso”, “Huba”, na kazi nyingine mbalimbali alizozifanya kupitia mtandao wa YouTube, ambazo zimekuwa zikiakisi maisha halisi na utamaduni wa Kitanzania.
Tuzo hii ni ishara ya ushirikiano wa kifilamu kati ya Tanzania na Nigeria ambao umeendelea kudumu kwa miaka mingi. Akizungumza baada ya kutunukiwa tuzo hiyo, Agness alieleza kuwa waandaaji wa tuzo hizo wamevutiwa na kazi za filamu kutoka Tanzania kutokana na utamaduni, amani, na ushirikiano unaoonyeshwa katika kazi hizo — mambo ambayo, kwa mujibu wake, ni alama ya utu na heshima ya Mwafrika, kama inavyoonekana kupitia tamthiliya maarufu ya “Kombolela”.
Aidha, Jumatatu, Oktoba 13, 2025, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD), amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Agness Suleiman Kahamba kuhusu mafanikio hayo na maendeleo ya sekta ya filamu nchini.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kasiga (PhD) alimpongeza Bi. Agness kwa juhudi zake katika kufanya kazi bora za filamu na kuiwakilisha vyema Tanzania katika majukwaa ya kimataifa ya filamu. Pia alimsihi aendelee kuonesha ubunifu, nidhamu, na weledi mkubwa katika kazi zake za sanaa ili kuutangaza vyema utamaduni wa Kitanzania ndani na nje ya nchi.
NDANI ya MSIKITI ALIOJENGA FARID MUSSA wa YANGA – AUPA JINA la MAMA YAKE – ”AISHA”…