Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amefunguka kuwa wakati anapewa jukumu la kuiongoza klabu hiyo, baadhi ya wanachama na mashabiki hawakuwa na imani naye kutokana na umri wake kuwa mdogo ukilinganisha na viongozi waliowahi kuiongoza timu hiyo hapo awali.
Akizungumza kuhusu safari yake ndani ya uongozi wa Yanga, Hersi alisema mashaka ya wanachama yalikuwa ya kawaida kwani wengi walikuwa wakijiuliza kama kijana kama yeye angeweza kuhimili presha na majukumu makubwa ya kuiongoza klabu yenye historia na mashabiki wengi kama Yanga SC.
“Ni kweli kulikuwa na mashaka, na niliyaelewa. Nilikuwa kiongozi kijana zaidi kuliko waliowahi kuongoza Yanga, hivyo ilikuwa rahisi kwa watu kutilia shaka uwezo wangu,” alisema Hersi.
Hata hivyo, aliongeza kuwa badala ya kuyumbishwa na maneno hayo, aliamua kuyatumia kama motisha ya kufanya kazi kwa bidii na kuonesha kuwa vijana pia wana uwezo mkubwa wa kuongoza na kufanya maamuzi makubwa yenye manufaa kwa klabu.
Chini ya uongozi wake, Yanga imeendelea kufanya mageuzi makubwa ndani na nje ya uwanja, ikiwemo kuongeza thamani ya kibiashara ya klabu, kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa kisasa ndani ya klabu.
Mashabiki na wadau wa soka sasa wanamtazama Hersi kama mfano wa viongozi vijana wanaoweza kuleta mabadiliko chanya katika michezo nchini.