

Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Amolo Odinga, amefariki dunia leo Jumatano, Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa zinaeleza kuwa Odinga alipata shambulio la moyo akiwa katika matembezi ya asubuhi katika Hospitali ya Macho na Kituo cha Utafiti cha Tiba Asilia cha Ayurvedic, kilichopo Koothattukulam, Wilaya ya Ernakulam, jimbo la Kerala nchini India, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Raila Odinga alikuwa mwanasiasa nguli ambaye maisha yake yalihusisha zaidi ya miongo minne ya mapambano ya kisiasa. Alikuwa mmoja wa wapigania demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya na aliwahi kuwekwa kizuizini mara kadhaa wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi.
Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Lang’ata mwaka 1992 na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Waziri wa Nishati, Waziri wa Barabara na Makaazi, na hatimaye kuwa Waziri Mkuu wa Kenya katika serikali ya mseto ya mwaka 2008 chini ya Rais Mwai Kibaki.
Raila amewania urais mara tano bila mafanikio, lakini amebaki kuwa nguzo kuu ya siasa za Kenya na mtetezi wa demokrasia, haki na umoja wa kitaifa.
Wakenya na viongozi kutoka mataifa mbalimbali wanaendelea kutuma salamu za rambirambi, wakimkumbuka kama shujaa wa mageuzi na kiongozi aliyejitolea kwa taifa lake.