*Aahidi Serikali kujenga Uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa wilayani Misenyi
*Agusia uboreshaji miundombinu katika bandari ya Bukoba na Kemondo
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kagera
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amehutubia maelfu ya wananchi wa Bukoba Mjini mkoani Kagera ambapo ameahidi kuwa Serikali imepanga kujenga uwanja mpya wa ndege cha kimataifa katika Mkoa huo.
Akizungumza leo Oktoba 16,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Kaitaba uliopo Bukoba Mjini mkoani Kagera Dk.Samia amesema ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa inatokana na sababu ya ufinyu wa kiwanja cha ndege Bukoba.
“Kwasababu ya ufinyu wa kiwanja cha ndege Bukoba, Serikali imejipanga kujenga uwanja mpya wa ndege cha kimataifa mkoani humo katika eneo Kyabajwa wilayani Missenyi.
Mgombea Urais Dk.Samia amesema uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa.
Kuhusu maboresho ya bandari katika Mkoa huo amesema Serikali imefanya ukarabati wa gati katika Bandari ya Kemondo kwa kuongeza kina na kuboresha gati hatua itakayosaidia meli kubwa kama Mv Mwanza kuweka nanga.
Ameongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ina miliki eneo la ekari 100 kwa ajili ya kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo ya maghala katika Bandari ya Kemondo.
Pia amesema Bandari ya Bukoba imefanyiwa marekebisho makubwa kwa kuhusisha ukarabati wa magati matatu, uchimbaji wa kina na ujenzi wa jengo jipya la abira lenye uwezo wa kuhudumia abiria 700.
Ameongeza ukarabati huo umehusisha ujenzi wa kizuizi cha upepo kusaidia upakiaji abiria na mizigo kwa usalama.
“Tumekarabati gati mbili kwa ajili ya vyombo vingine vidogo ambavyo hutoa huduma ziwani. Maboresho ya bandari yameleta meli kubwa za kisasa kama MV Mwanza ambayo imeanza kutoa huduma Mwanza – Kemondo – Bukoba.
Vilevile, amesema katika mkoa huo sekta ya uzalishaji imepewa kipaumbele kwa kuifanya sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 ifikapo 2030 kutoka asilimia sita ya sasa.
Katika sekta ya uvuvi, Dk. Samia amesema Serikali inakwenda kujenga mazingira mazuri kwa kuwapatia wavuvi mafunzo na nyenzo ikiwemo mitaji na vyombo vya kuvulia samaki.
Pia, ameeleza kuwa kupitia kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo na kuanzisha machinjio ya kisasa kuongeza ubora wa nyama kwa viwango vya kimataifa.
“Tunasoko kubwa ndugu zangu ulimwenguni, lazima tuingie kwenye viwango vya kimataifa ili tuweze kuuza mazao yetu yatokanayo na mifugo yetu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine amesema anafahamu changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo kukosa maeneo ya kufanyoa biashara zao.
“Kwasasa Serikali inajenga soko kubwa la wafanyabiashara hao Bukoba mjini eneo la Kishenye ambapo sh. bilioni 10 zimetengwa kukamilisha soko hilo.
Mgombea Urais Dk.Samia pia amesema Serikali itaendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri.
“Wale tunaolima kahawa tulime kwa wingi, tuuze kwa wingi halmashauri zikusanye fedha mfuko huo uongezeke,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa mkoa huo kuna mradi wa kimkakati wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
“Bomba hilo linapita Bukoba vijijini, Missenyi, Muleba na Biharamulo ambapo umetoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi katika hatua za awali.
“Serikali inatarajia mradi huo utatoa fursa nyingine wakati wa uendeshaji mradi huo hususan kupitia kampuni za utoaji huduma.”
Kwa upande wa miundombinu wezeshi alibainisha kuwa katika miaka mitano iliyopita serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la Kitengule linalounganisha barabara kuu ya Kyaka – Bukene – Benaco na barabara ya Kagera Sugar hadi Kakunyu.
Alisema kukamilika kwa daraja na barabara hizo kumewapunguzia wakulima wa miwa umbali wa kusafirisha malighafi kutoka kilometa 140 hadi kilometa 14.
“Walikuwa wanazunguka kilometa 140 sasa kilometa 14 miwa inafika ikiwa na hadhi yake ileile.
Katika miaka mitano inayokuja mkitupa ridhaa yenu tutaendelea kukamilisha barabara ya Lusahunga – Lusumo kwa sh. bilioni 153.5 ambapo umefikia asilimia 19.
Pia amesema miongoni mwa miradi mingine iliyopo katika ilani ni ujenzi wa barabara Murugalama – Lulenge – Nyakahura (km 85) na kujenga kwa lami barabara ya Bwajai – Kanyai hadi Buyangu pamoja na barabara za ndani eneo la Mutukula mjini.
Kuhusu mafuriko ya mara kwa mara katika Mto Kanoni, amebainisha tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za ujenzi wa kingo za mto huo ili kuondoa changamoto za mafuriko Bukoba mjini.