Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kagera.
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake itaongeza mabweni katika shule za sekondari ikiwemo maeneo ya visiwa ambapo wanafunzi wanapata shida kuvuka kwenda upande wa pili.
Akizungumza leo Oktoba 15,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Kaitaba uliopo Bukoba Mjini mkoani Kagera pamoja na mambo mengine amezungumzia mkakati huo wa kuongeza mabweni na shule za Sekondari katika maeneo ya visiwa katika Mkoa huo.
“Wale wanaokwenda kwenye visiwa wakute kuna mabweni na shule ili waweze kusoma vizuri. Tunaendelea kutunisha mfuko wa elimu ya juu ili wanaomaliza kidato cha sita wapate fursa kusoma elimu ya juu bila wazazi wao kuhangaika,” alisisitiza.
Akieleza zaidi kuhusu sekta ya elimu Dk.Samia amesema kuwa Serikali katika mkoa huo zimejengwa shule tatu za amali pamoja na shule moja ya sayansi ya wasichana.
Vilevile, alieleza kuwa serikali imejenga vyuo vya ufundi ikiwemo chuo cha VETA mkoa huku kwa upende wa vyuo vikuu imeanzishwa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Kagera.
Kuhusu umeme amesema Serikali imetekeleza ahadi ya kufikisha umeme kila kijiji kama Ilani ya uchaguzi iliyopita ilivyoelekeza.
“Katika miaka mitano ijayo, Serikali yake inakwenda kukamilisha kusambaza nishati hiyo katika vitongoji vyote kwani hadi sasa nusu ya vitongoji nchini vimeshafikishiwa huduma hiyo.
Dk. Samia alisema katika Mkoa wa Kagera kuna miradi minne mikubwa ya kimkakati ya kuzalisha umeme wa maji ambayo miradi hiyo imekamilika.
Pia amesema mradi wa Kakono -Missenyi upo katika hatua ya upembezi yakinifu huku serikali ikijipanga kujenga vituo vya kupokea na kupoza umeme ili kuongeza uhakika wa umeme kwa wananchi.
“Tunataka umeme upatikane mwaka mzima na kama ukizima basi iwe kwa sababu ya matengenezo kwenye mitambo lakini tuwe na uhakika wa umeme mwaka mzima.
“Tunataka umeme uwe wa kutosha kwa ajili ya kutekeleza mpango wa uanzishwaji kongani za viwanda na upatikanaji nishati safi ya kupikia,” alisisitiza.
Kwa upande wa maji amesema lengo ni kila Mtanzania apate huduma ya maji safi na salama huku akisisitiza kwamba huduma ya maji ni ya lazima na ndio maana Serikali inatumia mabilioni ya fedha kuhakikisha maji yanapatikana maeneo yote.