- LILONGWE: KOCHA Mkuu wa Yanga, Romain Folz, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi utakaochezwa Jumamosi.
Tayari kikosi cha Yanga kimewasili Malawi kwa ajili ya mchezo huo wa raundi ya kwanza kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi.
Folz amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji waliopo wanajituma kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika mchezo huo muhimu.
“Tunajua Silver Strikers ni timu bora, kama zilivyo timu nyingine zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Tumefanya uchambuzi wa kutosha na tunajua nini cha kutarajia, lakini kipaumbele chetu ni kuonesha mchezo wetu bora na kupata ushindi, tukiwaheshimu wapinzani wetu,” alisema Folz.
Akizungumzia hali ya wachezaji, Folz alisema ari na motisha ya timu inaongezeka kila siku, jambo analoliona kama sehemu ya mchakato wa maendeleo ya timu ya kitaalamu.
“Ni mchakato wa kawaida wa ukuaji. Tunajitahidi kuboresha kila siku na naamini katika wiki na miezi ijayo tutaendelea kuona maendeleo makubwa zaidi,” aliongeza.
Kuhusu mashabiki wengi wa Yanga wanaotarajiwa kusafiri kutoka Tanzania kwenda Malawi, Folz aliwatumia salamu za shukrani na hamasa, akisema licha ya kurudia mara nyingi maneno yake, ujumbe wake unabaki uleule — “kuwa na nguvu, tushirikiane na tuamini katika timu yetu.”
The post Folz: Tunaiheshimu Silver Strikers, lakini tunalenga ushindi first appeared on SpotiLEO.