DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amewataka wapenzi wa michezo nchini kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano ya kimataifa ya mpira wa kikapu Road to BAL yanayotarajiwa kufanyika kesho ( Leo Ijumaa) katika Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Dar es Salaam.
Mashindano hayo ya raundi ya awali yatashirikisha timu ya Dar City kutoka Tanzania, pamoja na timu kutoka Uganda na Visiwa vya Comoro. Timu mbili zitakazofanya vizuri zitasonga hatua ya 16 bora itakayochezwa Kenya au Afrika Kusini, ambapo timu nne bora zaidi zitafuzu hatua ya robo fainali.
“Mashindano haya si jambo dogo kwa mchezo wa kikapu. Ni fursa nyingine kwa Watanzania kujionea kwa macho yao mashindano yanayojumuisha mataifa mengine yakichezwa hapa nyumbani,” alisema Mwinjuma.
Ameeleza kuwa serikali inafurahia maendeleo ya mchezo wa kikapu nchini na kupongeza klabu ya Dar City kwa maandalizi bora na ushiriki wake wa kimataifa.
Mwinjuma aliongeza kuwa kuwepo kwa mchezaji wa Kitanzania kama nahodha wa timu hiyo ni jambo la kizalendo, akiwataka Watanzania kujitokeza kuisapoti timu hiyo kesho.
“Mmehakikisha mchezaji wa Kitanzania anakuwa nahodha. Nawaomba mashabiki wa michezo waje kwa wingi kushuhudia burudani hii ya kikapu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameipongeza Dar City kwa maendeleo yake akisema timu hiyo imeanza kuchukua sura ya kimataifa kutokana na uwepo wa kocha wa kigeni kutoka Senegal, Pabi Gueye.
“Tumezoea kuona timu zetu zikiwa na makocha wazawa, lakini sasa tunashuhudia timu inayokuwa na taswira ya kimataifa. Ni ishara nzuri kwa maendeleo ya mchezo wa kikapu nchini,” alisema Chalamila.
Ameongeza kuwa mchezo huo ni fursa ya kipekee kwa wananchi kushuhudia michezo ya kiwango cha juu na kuimarisha umoja wa kitaifa kupitia michezo.
Nahodha wa Dar City, Hasheem Thabit, alisema kikosi chake kimejipanga vizuri na kinatarajia kuonesha kiwango bora katika mashindano hayo.
“Tupo katika mazoezi ya mwisho na tunaomba Watanzania waje kutusapoti. Kikapu bado kinakabiliwa na changamoto za udhamini, lakini tumeendelea kupambana,” alisema Thabit.
Ameeleza kuwa yeye pamoja na Musa Mzenji wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika timu hiyo na kuhimiza wazazi kuwahamasisha watoto kushiriki katika michezo kwani ni ajira, ni maisha na sehemu ya makezi kwa vijana.
Naye Kocha wa Dar City, Pabi Gueye, alisema anafurahia kuwa sehemu ya timu hiyo na ameipongeza Tanzania kwa mazingira mazuri ya maandalizi.
“Nimefurahia sana kuwa Tanzania. Mazingira ni mazuri na timu iko vizuri. Naamini mashabiki watafurahia burudani tutakayoi ittoa kesho,” alisema.
Katika mashindano hayo mastaa mbalimbali wa mchezo huo kutoka Marekani na maeneo mengine watakuwepo wakiongozwa na mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Hasheem Thabit.
The post ‘Njoeni tuisapoti Dar City kesho’ first appeared on SpotiLEO.