Soka la Tanzania limeandika historia mpya baada ya klabu kongwe za Simba na Yanga kuingia katika orodha ya timu kumi bora za Afrika, kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde ya Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS). Mafanikio haya yanasisitiza ukuaji mkubwa wa soka la klabu nchini Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ripoti ya IFFHS, ambayo imeangazia matokeo na mafanikio yaliyopelekea ukusanyaji wa alama nyingi kwenye mashindano mbalimbali kuanzia Oktoba Mosi 2024 hadi Septemba 30, 2025, imeonyesha wazi ubora wa klabu hizi. Klabu ya Simba ndio pekee kutoka kanda ya Afrika Mashariki iliyoshika nafasi ya juu kabisa, ikikamata nafasi ya Tisa (9), huku watani wao wa jadi, Yanga, wakifuata nyuma yao kwa kushika nafasi ya Kumi (10).
Uwepo wa klabu hizi mbili katika ‘Top 10’ ya Afrika ni heshima kubwa, hasa ikizingatiwa kuwa zinashindana na vigogo wa soka la Afrika Kaskazini na Kusini.
Katika orodha hiyo inayoongozwa na klabu za Misri, Pyramids imeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Mabingwa wa Afrika, Al Ahly, ambao wamekaa nafasi ya pili. Klabu ya RS Berkane ya Morocco inashika nafasi ya tatu, huku Esperance ya Tunisia ikiwa nafasi ya nne na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikimalizia nafasi ya tano. Simba na Yanga zimeziacha nyuma klabu nyingine nyingi maarufu barani humo.
Kinachovutia zaidi katika mafanikio haya ya Simba ni ukweli kwamba, klabu hiyo haijabeba kikombe chochote cha maana cha kimataifa ndani ya kipindi hicho cha tathmini. Hii inaashiria kuwa uthabiti katika mashindano ya klabu barani Afrika, ikiwemo kufika hatua za juu, ndio umekusanya alama nyingi.
Wachambuzi wa soka wameanza kujiuliza kwa mshangao: Ikiwa Simba imeweza kupata nafasi ya Tisa bila kubeba taji la kimataifa, itakuwaje endapo itafanikiwa kubeba taji la Ligi Kuu ya NBC (NBCPL) msimu huu, au kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Afrika? Mafanikio haya ni ishara tosha kwamba soka la klabu nchini Tanzania limeingia katika ukurasa mpya wa ushindani barani Afrika.