Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajia kuendelea leo hii kwa michezo ya hatua ya awali mkondo wa kwanza kutimua vumbi huku macho ya Watanzania yakiwa kwa mwakilishi wa kwanza anayekipiga leo Nchini Malawi Yanga ambaye atakuwa ugenini kusaka tiketi ya hatua ya makundi dhidi ya Silver Strikers.
Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga Romain Folz amekiri kuwa maandalizi yote yamekamilika na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao hautakuwa mwepesi.
“Hakuna mchezo mrahisi au mpinzani mwepesi kwenye mashindano makubwa na tumejiandaa vizuri kwa hilo kwasababu kila mchezo ni muhimu na ndiyo namna tutauendea mchezo wa kesho kuhakikisha tunaondoka hapa na matokeo mazuri”Amesema Folz.
Mchezo huo utapigwa katika uwanja wa Taifa wa Bingu, Malawi majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuchezwa Oktoba, 25, 2025 katika dimba la Benjamin Mkapa.