
WANANCHI wa Kijiji cha Karema wilayani Tanganyika, mkoani Katavi, wameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajengea kizimba maalum pembezoni mwa Ziwa Tanganyika ili kukabiliana na changamoto ya mamba waliokuwa wakiwaua na kuwajeruhi wananchi kwa muda mrefu.
Shukrani hizo zilitolewa Oktoba 17, 2025, wakati wa usimikaji wa kizimba hicho kilichojengwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa lengo la kupunguza migongano kati ya binadamu na mamba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Idara ya Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Tanganyika, Bruno Nicolaus, ameishukuru TAWIRI kwa jitihada zao za kulinda maisha ya wananchi wanaoishi kandokando ya ziwa hilo.
“Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha usalama wa wananchi unaimarishwa. Tutaweka sheria ndogo ndogo kuhakikisha kizimba hiki kinatunzwa na kutumika ipasavyo,” amesema Nicolaus.
Kwa upande wake, Mtafiti na Msimamizi wa Ujenzi wa Vizimba kutoka TAWIRI, Selemani Moshi, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu tabia za mamba na namna bora ya kutumia kizimba hicho kwa usalama.
“Wananchi wanapaswa kuepuka kutupa taka au mabaki ya chakula ziwani kwani huchochea mamba kusogea karibu na maeneo ya shughuli za binadamu. Pia wasifanye kazi majini nyakati za jioni,” amesisitiza Moshi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Karema, Juma Iddi ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TAWIRI kwa kusaidia ujenzi wa kizimba hicho, akiahidi kuwa watahakikisha kinatumika ipasavyo.
“Tulikuwa tunaishi kwa hofu kubwa, hasa wanawake na watoto waliokuwa wakifanya shughuli ziwani. Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kutuondolea adha hii ya muda mrefu,” amesema Iddi.
MWANZA: JESHI la ZIMAMOTO na UOKOAJI YAPOKEA MAGARI MAPYA, ACF MUGISHA AELEZA kwa UNDANI