

Tume ya Uchaguzi ya Uganda imetangaza rasmi tarehe 15 Januari 2026 kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu wa taifa hilo, ambapo Rais Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kugombea tena, akitaka kuongeza muda wa utawala wake hadi kufikia karibu nusu karne madarakani.
Museveni, ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986, kwa sasa ndiye kiongozi wa nne barani Afrika aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi. Serikali yake imewahi kubadilisha Katiba mara mbili — kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais na kuondoa mipaka ya mihula ya urais, jambo lililomruhusu kuendelea kugombea bila kizuizi cha kisheria.
Kama ilivyokuwa katika Uchaguzi wa mwaka 2021, mpinzani mkuu anatarajiwa kuwa mwanasiasa na msanii mashuhuri Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana kupitia harakati zake za kisiasa na muziki wa kijamii.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, Museveni alipata asilimia 58% ya kura, huku Bobi Wine akipata 35%. Hata hivyo, Wine alidai ushindi wake uliibiwa, madai ambayo Tume ya Uchaguzi ilikanusha, ikisisitiza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Uchaguzi wa mwaka 2026 unatarajiwa kuwa jaribio lingine la kisiasa litakalopima ushawishi wa Museveni kwa kizazi kipya cha vijana, na uthabiti wa demokrasia nchini Uganda baada ya zaidi ya miaka 40 ya utawala wa chama chake, National Resistance Movement (NRM).
VIDEO INAYOTREND ya MAMA AKIPIGWA VIBAO na MWENZAKE ENEO la BIASHARA – WAZIRI GWAJIMA ANAMTAFUTA….