Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Mkoa wa Ruvuma Rashid Mchekenje akitoa taarifa ya kikao kazi cha walimu wanawake kilichofanyika katika Ukumbi wa Chama cha akiba na mikopo(Saccos)Manispaa ya Songea jana,katikati Mwenyekiti wa Chama hicho Kalimeje Sandali na kulia Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro.
Waziri wa sheria na katiba Dkt Damas Ndumbaro katikati, akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Mkoa wa Ruvuma.
………….
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
WAZIRI wa Sheria na Katiba Dkt Damas Ndumbaro,amewataka Watanzania kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kujiletea maendeleo,na kuepuka kusambaza na kuchapisha habari za uzushi zinazokashifu na kudhalilisha Viongozi na Serikali iliyopo madarakani.
Dkt Ndumbaro amesema hayo jana,wakati akizungumza na walimu wa shule mbalimbali za msingi na sekondari za Mkoa wa Ruvuma kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chama cha walimu Songea Manispaa eneo la Majengo kata ya Majengo Wilayani Songea.
Dkt. Ndumbaro amesema,mitandao ya kijamii ina manufaa makubwa,lakini kama ikitumika kinyume mtu anaweza kujikuta kwenye mgogoro mkubwa na mamlaka za nchi kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Mnavyotumia mitandao mfahamu wazi kwamba kuna sheria na makosa mtandao ya mwaka 2015,kuna sheria ya Takwimu,kuna sheria ya huduma za vyombo vya Habari ya mwaka 2016,lakini kuna kanuni za maudhui mitandaoni kwa hiyo lazima watu wafahamu”alisema Dkt Ndumbaro.
Dkt Ndumbaro, amewaomba walimu kusadia kuielimisha jamii ambayo inaendelea kupotoshwa na taarifa za uongo na chuki zinazoandikwa mitandaoni ambazo hazina ukweli na zinalenga kuwagombanisha wananchi na Serikali yao.
“kwenye mitandao ya kijamii kuna taarifa nyingi zenye kuleta chuki ili kuifanya nchi yetu isitawalike,tukifikia hatua hiyo kazi zenu hazitafanyika mtakimbia,hata anayewalipa mshahara kila mwezi naye atakimbia,Serikali inawaomba sana isaidieni kuielimisha jamii kuhusu maadili na matumizi mazuri ya mitandao”alisisitiza Ndumbaro.
“Katika siku za hivi karibuni katika mji wetu wa Songea kulikuwa na taarifa ya kupotea kwa Padre,kuna tofauti kubwa kati ya kupotea na kutekwa,unaposema mtu ametekwa maana yake umeona kile kitendo na una uhakika nacho kwamba Damas amekwenda kwa Sandali amemchukua kwa nguvu,amemmfunga kamba au pingu,amemtesa na ameondoka naye uko ndiyo kutekwa”alisema.
“Kwa hiyo mtu hasipojulikana amekwenda wapi huo sio utekaji bali mtu amepotea,lakini tumepata taarifa kwamba huyo Padre amepatikana na hakutekwa bali alipotea kwa sababu zake mwenyewe”.
Alisema, baadhi ya watu wanaojiita wana harakati wanatumia mitandao ya kijamii kuleta taaluki katika nchi yetu na kupandikiza chuki kati ya jamii na Serikali kwa sababu wanazozifahamu mwenyewe.
Amewaomba walimu, kuendelea kuisaidia Serikali katika kuelimisha jamii ambayo inapotoshwa na taarifa ambazo hazina ukweli hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Katika hatua nyingine Dkt Ndumbaro,amewaomba walimu na viongozi wa makundi mbalimbali kuelimisha jamii umuhimu wa kulinda amani tuliyoachiwa na Waasisi wetu Mwalimu Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Walimu(CWT)Mkoa wa Ruvuma Mwalimu Rashid Mchekenje alisema, katika kikoa hicho viongozi wa walimu wanawake na walimu kwa ujumla wamejengewa uwezo,historia ya chama cha walimu umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
Aidha Mchekenje alitaja mambo mengine waliyofundishwa walimu hao ni pamoja na ujasiri kama viongozi wa kike na kuipitia sera ya jinsia na walimu wanawake ambao wana jukumu kubwa la kuwalinda watoto wa kike hasa kwenye vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoani Ruvuma Kalimeje Sandali alisema,wataendelea kutoa elimu kwenye shule zote za msingi na Sekondari kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na umuhimu wa kulinda amani.
Sandali alisema,wana wajibu mkubwa kuungana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika shughuli zake kwani katika kipindi cha miaka minne chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,imefanyia kazi changamoto nyingi zinazowakabili walimu.
“Tunajua haiwezekani kutatuliwa mambo yote kwa wakati mmoja,lakini tumeona na kushuhudia jitihada mbalimbali za Serikali ikiwemo changamoto ya upungufu wa walimu ambayo Serikali imetoa kibali cha kuajiri walimu wapya”alisema Sandali.








