DAR ES SALAAM: KUELEKEA mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Flambeau du Centre FC ya Burundi, kikosi cha Singida Black Stars kimepania kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kuhakikisha kinatinga hatua ya makundi.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Bujumbura, Burundi.
Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, amesema maandalizi yamekamilika na wachezaji wako tayari kwa vita ya kusaka ushindi muhimu.
“Tunajua ubora na udhaifu wa mpinzani wetu kwa sababu tumeshacheza nao mechi ya kwanza. Tumefanyia kazi maeneo yote na kesho tutatumia madhaifu yao kutafuta ushindi,” alisema Gamondi.

Nahodha wa timu hiyo, Hussein Masalanga, amesema morali ya wachezaji ipo juu na kila mmoja anatambua umuhimu wa mchezo huo kwa historia ya klabu.
“Sisi wachezaji maandalizi tulianza siku ile baada ya mchezo kumalizika dhidi ya wapinzani wetu. Hakuna mchezaji mwenye presha, wote tupo tayari kupambana kesho kuiandikia timu historia ya kuingia hatua ya makundi,” alisema Masalanga.
Mashabiki wa Singida Black Stars wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao, ikiwa na malengo ya kuipa heshima Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.
The post Singida Black Stars waapa kufanya vyema nyumbani first appeared on SpotiLEO.








