NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGOMBEA Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo tayari amepiga kura katika kituo cha kupigia kura VETA kilichoko katika kata ya Kwakilosa Mjini Iringa.
Ngajilo amefika katika kituo hicho saa 4.30 asubuhi ya leo Jumatano, Oktoba 29, 2025 akiwa ameongozana na watu mbalimbali waliojitokeza kupiga kura katika kituo hicho.
Baada ya kufika katika kituo hicho, alipanga foleni katika mistari ya wananchi ambao nao walikuwa kwenye foleni kwa ajili ya kupiga kura na kisha kukaribishwa na mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi na kisha kuingia ndani kwa ajili ya kupiga kura kwa ajili yake, urais na diwani wa kata ya Kwakilosa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura, Ngajilo anayegombea nafasi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuitafuta kwa miaka 15, Ngajilo alisema kuwa anashukuru kuwa mmoja ya wapiga kura na kutumia nafasi yake ya kikatiba na kwamba amefurahishwa kuona wananchi wamejitokeza kwa wingi kupiga kura.
Alisema kuwa pongezi kwa tume huru ya uchaguzi kwa maandalizi mazuri kwani ametembelea vituo vyote jimboni hili na kuona utaratibu ulivyokuwa mzuri na uchaguzi uko wa amani na utulivu.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi ambao bado wapo nyumbani wajitokeze kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowatumikia kwa kipindi cha miaka mitano kwani kuna la kujivunia katika kupiga kura kwa ajili ya kupata kiongozi atakayekuongoza na wakumbuke kila mamlaka inatoka kwa Mungu.
Aidha amepongeza amani ambayo imetawala kuanzia mwanzo wa zoezi la kupiga kura na kuwasisitiza wananchi ambao bado waende vituoni kwani ni haki ya kila mwananchi.







