RIYARDH: MCHEZAJI nyota wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, amefichua kifaa cha kifahari zaidi kuwahi kukinunua maishani mwake kuwa ni ndege binafsi aina ya Bombardier Global Express 6500 yenye thamani ya euro milioni 50 ambayo ni sawa na zaidi ya bilioni 145 za Kitanzania.
Katika mahojiano maalum kwenye kipindi cha Piers Morgan Uncensored, nahodha huyo wa Al-Nassr mwenye umri wa miaka 40 alizungumzia kuhusu anasa, nidhamu na mafanikio yake ya kifedha, huku akifananisha kuwa bilionea na kushinda tuzo ya kifahari zaidi katika soka Ballon d’Or.
Ronaldo, ambaye thamani yake ya mali iliripotiwa kufikia dola bilioni 1.4 mnamo Oktoba 2025 baada ya kusaini mkataba wenye thamani kubwa zaidi katika historia ya michezo, kwa sasa anapata mshahara wa takribani pauni milioni 178 kwa mwaka. Mkataba huo pia unajumuisha pauni milioni 24.5 kama ada ya usajili, jambo lililomfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa soka kufikia hadhi ya bilionea rasmi.
“Ndege yangu binafsi ndiyo kitu cha gharama zaidi nilichowahi kununua” Ronaldo alifichua kuwa ingawa ana uwezo wa kununua chochote anachotaka, huwa anatumia fedha zake kwa umakini.
“Kitu cha gharama zaidi nilichowahi kununua? Ndege. Nilikuwa nayo tangu nikiwa na miaka 30, lakini mwaka jana niliibadilisha, na ilikuwa ghali sana,” alisema na kuongeza: “Naweza kununua ninachotaka, lakini sihitaji kila kitu.”
Ronaldo pia alizungumza kuhusu mapenzi yake kwa magari ya kifahari, akifichua kuwa sasa anayachukulia zaidi kama uwekezaji kuliko kuwa kama anasa.
“Sijui hata nina magari mangapi. Kwa makadirio, labda 41 au 42,” alisema kwa tabasamu. “Ninapenda Bugatti ni magari ya kipekee lakini siku hizi siendeshi sana. Magari hayaninogei kama zamani.”
Akitafakari mafanikio yake kifedha, Ronaldo alisema kufikia kiwango cha bilionea ni moja ya malengo yake binafsi nje ya uwanja wa soka.
“Kufikia hadhi ya bilionea kulihisi kama kushinda Ballon d’Or,” alisema. “Sina uraibu wa pesa, lakini nilifurahia kufikia hatua hiyo. Ilikuwa moja ya malengo yangu, pamoja na kushinda makombe, Ballon d’Or na Ligi ya Mabingwa. Nilipofikisha miaka 39, nilikuwa nimefanikisha yote — nilijivunia sana.”
Ronaldo pia alizungumzia mipango yake baada ya kuachana na soka, akisema anaendelea kujiandaa kisaikolojia kwa kipindi hicho kigumu.
“Itakuwa ngumu, labda nitalia mimi huwa nalia kirahisi,” alikiri. “Lakini nimekuwa nikijiandaa tangu nikiwa na miaka 25. Nitatumia muda zaidi na familia, kuangalia michezo kama UFC, kucheza padel, na kuendeleza biashara zangu. Sitakuwa YouTuber, lakini nitachunguza mambo mengine.”
Kwa sasa, mshambuliaji huyo mkongwe anatarajiwa kurejea uwanjani Jumatano ijayo, wakati Al-Nassr watakapovaana na FC Goa ya India katika michuano ya AFC Champions League Two mjini Riyadh.
Ronaldo anaendelea kudhihirisha kuwa mafanikio yake hayapo tu ndani ya uwanja, bali pia nje yake akithibitisha kwa mara nyingine kuwa nidhamu, bidii, na imani vinaweza kumuinua mtu hadi kilele cha dunia.
The post Cristiano Ronaldo alinunu ndege yake binafsi kwa bilioni 145 first appeared on SpotiLEO.



