GENOA: KLABU ya Genoa imemtangaza Nyota wa zamani wa AS Roma na mshindi wa kombe la Dunia 2006 na Italia Daniele De Rossi kuwa kocha mpya wa timu hiyo ya Serie A, muda mfupi baada ya kumfukuza kazi Patrick Vieira, ikiwa ni hatua za kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
Vieira, raia wa Ufaransa, alitimuliwa kufuatia mwanzo mbaya wa msimu ambapo Genoa haikushinda mechi yoyote, ikirekodi sare tatu na vipigo sita, hali iliyowaacha wakiburuza mkia wa msimamo wa ligi kuu ya Italia Serie A.
Wikiendi iliyopita kocha wa muda wa klabu hiyo Domenico Criscito aliiwezesha kupata ushindi wake wa kwanza wa msimu huu Genoa ikiilaza Sassuolo mabao 2–1 matokeo yaliyowapandisha hadi nafasi ya 18, wakiwa na pointi sita, sawa na Pisa walioko kwenye eneo salama.
“Genoa CFC inatangaza rasmi kuwa Daniele De Rossi ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa kikosi cha kwanza,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
De Rossi mwenye umri wa miaka 42, ambaye alitumikia AS Roma kwa takriban miaka 20 kama mchezaji, alipata kazi yake ya kwanza ya ukocha wa timu ya wakubwa ya AS Roma Januari 2024 baada ya Jose Mourinho kufutwa kazi.
Aliongoza Roma kumaliza nafasi ya sita kwenye Serie A na kufika nusu fainali ya Europa League, kabla ya kusaini mkataba wa hadi mwaka 2027.
Hata hivyo, De Rossi alitimuliwa Septemba mwaka jana kufuatia mwanzo mbaya wa msimu mpya, na mchezo wake wa mwisho ukiishia kwa sare ya 1–1 dhidi ya Genoa timu ambayo sasa anayorejea kuinoa.
Genoa watakuwa na mtihani mgumu kwenye mchezo wao ujao nyumbani dhidi ya Fiorentina, ambao nao wako katika hali ngumu baada ya kumfuta kazi Stefano Pioli Jumanne, kufuatia matokeo mabaya yaliyowaacha mkiani mwa Serie A.
The post Genoa yampa kazi De Rossi first appeared on SpotiLEO.



