NI wazi kuwa Singida Black Stars ambayo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake miaka tisa iliyopita wakati huo ikiitwa Ihefu SC, ina mlima mrefu wa kupanda katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayoanza Novemba 21.
Singida Black Stars imepangwa katika kundi C lililo na wapinzani wakubwa wenye uzoefu wa michuano ya Afrika, CR Belouizdad (Algeria), Stellenbosch FC (Afrika Kusini) na AS Otoho (Kongo-Brazzaville).
Pamoja na kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Singida Black Stars kushiriki michuano hiyo na kufika hatua ya makundi kikosi chao kinajivunia uwepo wa wachezaji wenye uzoefu na michuano hiyo kama vile Clatous Chama na Khalid Aucho, hivyo wanaweza kutoa changamoto kwenye kundi hilo.
CR BELOUIZDAD (ALGERIA)
Hii ni klabu kongwe na yenye mafanikio Afrika. CR Belouizdad ilianzishwa mwaka 1962 jijini Algiers, ikiwa ni moja ya timu zilizochangia katika maendeleo ya soka la Algeria baada ya uhuru.
Hadi sasa, imetwaa mataji 10 ya Ligi Kuu ya Algeria kwenye misimu ya 1964-65, 1965-66, 1968-69, 1969-70, 1999-2000, 2000-01, 2019-20, 2020-21, 2021-22 na 2022-23.
Katika kumbukumbu zao, ushindi wao mkubwa zaidi katika historia ya michuano ya CAF ulikuwa mwaka 1996 walipoichapa Horoya AC ya Guinea kwa mabao 5-2. Hata hivyo, walipokea kipigo kikubwa zaidi 2001 walipofungwa mabao 7-0 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Mafanikio yao makubwa zaidi barani Afrika yalikuwa mwaka 1996, walipofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Washindi wa Afrika (Africa Winners Cup) kabla ya kutolewa na AC Sodigraf ya DR Congo.
Tangu hapo, Belouizdad imeendelea kuwa kati ya timu zenye ushindani mkubwa katoka ukanda wa Afrika Kaskazini. Klabu hiyo pia imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa timu ya taifa ya Algeria kwa kuzalisha wachezaji wanaopewa nafasi katika kikosi cha Mbweha hao wa Jangwani.
Miongoni mwa wachezaji hatari kwenye kikosi hicho ni pamoja na Youcef Laouafi mwenye mabao matatu kwenye ligi yao ya ndani na Abdennour Belhocini mwenye mabao mawili wote hao ni washambuliaji. Pia kikosi chao kina kiungo Mualbania, Endri Cekici.
STELLENBOSCH FC (AFRIKA KUSINI)
Licha ya kuwa na umri sawa na Singida BS, wawakilishi hawa kutoka Magharibi mwa Afrika Kusini huu ni msimu wao wa pili katika michuano ya kimataifa, ikumbukwe kuwa msimu uliopita walicheza nusu fainali ya michuano hii na Simba.
Timu hiyo changa, ilitupwa nje katika hatua hiyo kwa matokeo ya jumla ya bao 1-0, Simba iliibuka na ushindi huo nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan kabla ya kukomaa na kutoka suluhu Afrika Kusini.
Stellenbosch ilianzishwa mwaka 2016 na imepanda kwa kasi kwenye chati ya soka la Afrika Kusini, ndani ya miaka tisa, mwaka 2023 imebeba Kombe la Carling Knockout na kushika nafasi ya pili mara mbili kwenye Kombe la MTN 8 miaka miwili iliyopita baada ya kupoteza fainali zote mbili mbele ya Orlando Pirates, 2024 kwa mabao 3-1 na 2025 kwa mabao 3-0.
AS OTOHO (CONGO -BRAZZAVILLE)
Klabu hii kutoka Oyo, Congo-Brazzaville imekuwa nguzo ya mafanikio katika soka la Congo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Ilianzishwa mwaka 1998 na imekuwa bingwa wa ligi ya ndani mara sita (2018, 2018-19, 2019-20, 2021, 2021-22, 2023-24) huku ikishiriki michuano ya CAF mara saba, zikiwamo mara tano upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo waliishia hatua za awali kwenye miaka ya 2018, 2019, 2020, 2021 na 2022 huku upande wa Shirikisho hii ikiwa ni mara yao ya tatu kufika hatua ya makundi.
Katika awamu mbili zilizopita, walifika na kuishia hatua hiyo ilikuwa ni msimu wa 2018-19 na 2021-22.
AS Otoho inanolewa na kocha Christophe Mulumba ambaye amejijengea sifa kwa kuunda kikosi kinachocheza soka la kujilinda zaidi (compact defending) na kushambulia kwa kushtukiza.
The post HUU HAPA ‘MLIMA WA MIIBA’ WA SINGIDA BS CAF MSIMU HUU…WAKIPITA TU WAMETOBOA…. appeared first on Soka La Bongo.



.jpg)