Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCU LTD)Marcelino Mrope akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa zao la Korosho uliofanyika hivi karibuni.
Wadau wa zao la korosho wakiwa katika moja ya vikao kazi kwa ajili ya kujadili mwenendo wa kuboresha zao hilo.
………….
Na Mwandishi Wetu, Tunduru.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mnada wa kwanza wa zao la Korosho kwa msimu wa mauzo 2025/2026 chini ya usimamizi wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD).
Akizungumza ofisini kwake Mjini Tunduru Meneja Mkuu wa Chama hicho Marcelino Mrope amesema,katika msimu wa 2025/2026 mnada wa kwanza utafanyika Tarehe 12 Jumatano katika Chama cha Msingi cha Ushirika Namitili(Amcos) kilichopo Kijiji cha Nakapanya Tarafa ya Nakapanya Wilayani humo.
Amesema kuwa,awali mnada huo ulitakiwa kufanyika wiki iliyopita lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao ikiwemo kukosekana kwa mtandao unaotumika kwenye uendeshaji wa minada ya mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Amesema,katika msimu 2025/2026 korosho zitauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani chini ya Usimamizi wa soko la bidhaa Tanzania(TMX) na hakuna mfanyabiashara au kampuni itakayoruhusiwa kununua korosho majumbani badala yake wafike kwenye minada.
Mrope,amewataka wakulima kuhudhuria kwa wingi katika mnada huo ili wapate kufahamu mwenendo mzima wa soko,utaratibu utakaotumika katika kuuza korosho msimu 2025/2026 na mambo mengine muhimu yanayohusu zao hilo.
Mrope amesema,katika msimu 2025/2026 wamejipanga kumaliza changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika msimu wa 2023/2024/2024/2025 ikiwemo upungufu wa magunia na vifaa vingine vinavyotumika kwenye uendeshaji wa minada ya korosho.
“Lengo ni kutaka kuhakikisha wakulima wote wanakusanya korosho zao kwa wakati na kuzifikisha kwenye maghala ya vyama vyao vya msingi vya ushirika vilivyopo kwenye maeneo yao kwa ajili ya minada,natumia nafasi hii kuwasisitiza wakulima waendelee kukusanya korosho na wazingatie ubora ili wapate bei nzuri”amesema Mrope.
Amesema hadi sasa wamefanikiwa kupata gunia 600,000 zenye uwezo wa kuhifadhi kilo 48,000,000 ambazo zimesambazwa kwenye vyama mbalimbali vya msingi vya ushirika na mahitaji ya gunia kwa wakulima ni 437,500.
Kwa mujibu wa Mrope,usambazaji wa gunia kwenda kwa vyama vya msingi vya ushirika ulifanyika kwa awamu na katika awamu ya kwanza wamesambaza gunia zaidi ya gunia 300,000 kwa Amcos zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma na mikoa ya Njombe na Mbeya ambayo inayohudumiwa na TAMCU.
Aidha amesema,katika msimu wa mauzo 2025/ 2026 Chama Kikuu (TAMCU) kimepanga kukusanya zaidi ya tani korosho 35,000 za korosho ambazo ni sawa na kilo 35,000,000 ikiwa ni ongezeko la kilo 3,391,962 zilizokusanywa katika msimu wa 2024/2025.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa viuatilifu bure pamoja na mabomba ya kupulizia dawa za korosho kwa bei ya ruzuku kwa wote wakulima wanaojihusisha na kilimo cha zao hilo ili kuwapunguzia wakulima mzigo mkubwa wa kuhudumia mikorosho yao.
Amesema,wakulima wamenufaika na utaratibu wa upatikanaji wa pembejeo hizo ambapo kilo milioni 5,962,550 za Salfa ya unga imesambazwa,viuatilifu vya maji lita 270,573 na sumu ya kudhibiti wadudu lita 110,432.
Mrope amesema,uzalishaji wa zao la korosho unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na wadau wote kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya za hilo hasa upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za ugani.
Amesema, kuanzishwa na kusimamia kikamilifu mfumo wa stakabadhi ghalani umewezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei kubwa ambapo msimu uliopita bei wastani ilikuwa Sh.2.942.75 kwa kilo moja.
Amesema,mafanikio yaliyopatikana katika msimu 2024/2025 yametokana na maboresho ya sheria,kanuni na miongozo ya utekelezaji wa mfumo wa mauzo wa stakabadhi ghalani kwenye zao hilo chini ya usimamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania(TMX).
Mkulima wa korosho wa Kijiji cha Malumba Abdala Kawanga,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya kilimo kuwajali wakulima kwa kuwapatia pembejeo bure hali iliyosaidia kulima kwa tija na kuongezeka kwa uzalishaji mashambani.
Ameiomba Serikali,kuhakikisha inasimamia soko la korosho kwa kuwashawishi wanunuzi kutoa bei nzuri ili kuhamasisha wakulima waendelee na uzalishaji wa zao hilo ambalo linamchango mkubwa kiuchumi wa Wilaya ya Tunduru,Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.






