LUXEMBOURG CITY: Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joshua Kimmich, hatacheza katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Luxembourg utakaopigwa kesho Ijumaa, baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu wa kulia na kuondolewa kikosini.
Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) limetoa taarifa leo likithibitisha kuwa kiungo huyo wa Bayern Munich ameondolewa kwenye kikosi kutokana na jeraha hilo, lakini huenda akarudi uwanjani Jumatatu wakati Ujerumani watakapovaana na Slovakia nyumbani.

Kimmich, mwenye umri wa miaka 30, anaungana na Nico Schlotterbeck na Nadiem Amiri kwenye orodha ya wachezaji majeruhi katika kikosi cha kocha Julian Nagelsmann, huku mshambuliaji Karim Adeyemi akikosa mchezo wa Ijumaa kutokana na kufungiwa.
Ujerumani pia inawakosa nyota kadhaa akiwemo Kai Havertz, Jamal Musiala, Marc-Andre ter Stegen, Antonio Rudiger, Niclas Fuellkrug na Tim Kleindienst.
Ujerumani wako pointi sawa na Slovakia katika kundi lao la kufuzu Kombe la Dunia, lakini wanaongoza kwa tofauti ya mabao. Ni kinara wa kundi pekee itakayojihakikishia nafasi ya moja kwa moja katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Marekani, Mexico na Canada mwakani.
The post Kimmich aondolewa kikosini Ujerumani first appeared on SpotiLEO.







