BAADA ya msimu uliopita Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, msimu huu ina kibarua kingine kizito cha kuisaka fainali upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni siku chache tu tangu kupangwa kwa makundi ya michuano hiyo.
Kabla ya kufika fainali, Simba ambayo ipo kundi D sambamba na Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia, Petro Atletico (Angola) na Stade Malien (Mali), itakuwa na viunzi vitatu mbele yake ambavyo itatakiwa kuvivuka ikiwa chini ya Meneja Mkuu, Dimitar Pantev.
Viunzi hivyo ni kuvuka hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kumaliza kinara au kushika nafasi ya pili, baada ya hapo kingine kitakuwa hatua ya robo fainali ambapo imekuwa ikikwama kila iliposhiriki Ligi ya Mabingwa, kisha nusu fainali.
Ndani ya misimu saba ya mwisho kwa Simba kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, imefika robo fainali mara nne, ilikuwa 2018-19, 2020-21, 2022-23 na 2023-24, hivyo ina kibarua kizito cha kufanya ili kuweka rekodi mpya katika michuano hiyo.
Pamoja na hayo, hawa ndio wapinzani wa Simba katika kundi D, ilikuwaje hadi kutinga hatua ya makundi na historia yao ilivyo katika michuano hiyo ambayo wababe ni Al Ahly waliotwaa taji hilo mara 12.
ESPERANCE
Ni moja ya klabu kongwe na yenye heshima kubwa barani Afrika. Esperance ilianzishwa mwaka 1919 mjini Tunis, ikiwa na historia ndefu ya mafanikio katika soka la Tunisia na Afrika.
Hadi sasa, imetwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Afrika (1994, 2011, 2018 na 2019), ikicheza fainali tisa. Kwenye viwango vya CAF, Esperance imekuwa kati ya timu tano bora kila mwaka tangu 2010.
Ni klabu iliyo na nidhamu ya kiutawala, mfumo wa akademi na mashabiki wanaojulikana kwa namna ambavyo wamekuwa wakiisapoti timu hiyo kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi. Hii ni kati ya timu zenye nguvu kubwa ya mashabiki.
Kwenye orodha ya IFFHS, Esperance inashika nafasi ya saba kati ya klabu bora za Afrika kwa karne ya 20, huku CAF ikiitaja kama klabu ya tano bora ya karne mwaka 2000. Mwaka 2018, iliongoza orodha ya klabu bora Afrika kwa alama za CAF kitu kinachoonyesha ubora wake wa muda mrefu.
Kikosi chao cha sasa kinasimamiwa na Maher Kanzari, kocha mzawa anayetumia mfumo wa 4-2-3-1. Wachezaji muhimu ni Achref Jabri mwenye mabao saba kwenye ligi, kiungo mshambuliaji raia wa Brazil, Yan Sasse.
PETRO DE LUANDA
Ilianzishwa mwaka 1980, klabu hiyo inamilikiwa na kampuni ya mafuta ya serikali nchini Angola. Hadi sasa imetwaa mataji 19 ya ligi ya ndani na imekuwa bingwa wa Kombe la Angola mara 15.
Petro imekuwa ikipanda chati kwa kasi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikifika nusu fainali msimu wa 2021-22 na robo fainali 2023-24.
Kwa misimu mitatu mfululizo, imekuwa moja ya timu zinazocheza soka lenye mvuto, ikitegemea kasi, nguvu na nidhamu ya mbinu.
Kocha wao, Franc Artiga, ni Mhispania aliyepita Barcelona mwenye falsafa ya soka la kushambulia kupitia pembeni na pasi fupi. Hutumia mfumo wa 4-3-3 unaotoa nafasi kwa washambuliaji wake kufanya kazi kwa uhuru mkubwa.
Miongoni mwa nyota wa timu hiyo ni Tiago Azulao, mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa aliyeweka rekodi ya mabao zaidi ya 100 tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2016.
Petro ni timu yenye uwezo mkubwa wa kutawala mechi za nyumbani, uwanja wao wa 11 de Novembro wenye uwezo wa kuingiza mashabiki zaidi ya 48,000, umekuwa ngome yao ya ushindi katika michuano hiyo ya kimataifa.
Simba inatakiwa kuwa nao makini hasa katika mechi ambayo watacheza ugenini kwani mara nyingi hufunga mabao ndani ya dakika 30 za mwanzo. Hata hivyo, timu hii imekuwa na changamoto inapocheza ugenini.
STADE MALIEN
Klabu hii kutoka Bamako nchini Mali, ilianzishwa mwaka 1960, inashikilia rekodi ya kuwa klabu iliyotwaa mataji mengi zaidi ya Ligi Kuu ya Mali ambayo ni 23.
Mafanikio yake makubwa zaidi kimataifa yalikuwa mwaka 2009 ilipotwaa Kombe la Shirikisho Afrika, ikiiwakilisha Afrika Magharibi kwa mafanikio makubwa. Ni timu yenye utamaduni wa kukuza vijana kupitia akademi yao maarufu, Academie Jean-Marie Guindo, ambayo imezalisha wachezaji kama Seydou Keita ambaye aliwahi kutamba akiwa na Barcelona pamoja na Adama Coulibaly aliyezichezea Lens, Auxerre na Valenciennes zote za Ufaransa. Kipa wa Yanga, Djigui Diarra anatokea katika timu hii.
Stade Malien hutumia mfumo wa 4-4-2. Hii ni timu ambayo mara nyingi haina wachezaji wenye majina makubwa, lakini hutegemea uchezaji wa pamoja kama timu.
Hucheza mechi zake za nyumbani kwenye Uwanja wa Stade du 26 Mars, uliopo katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Bamako.
The post BAADA YA MSIMU ULIOPITA KUISHIA FAINAL…KIBARUA KIGUMU CHA SIMBA CAF HIKI HAPA…. appeared first on Soka La Bongo.


