DAR ES SALAAM: GOLIKIPA namba moja wa Simba SC, Moussa Camara, anatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea Morocco kwa ajili ya kufanyiwa matibabu na upasuaji wa goti, ambao umepangwa kufanyika Jumatatu, Novemba 17.
Camara alipata majeraha hayo wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, ambapo alilazimika kutolewa nje baada ya kugongana na mshambuliaji wa wapinzani.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa upasuaji huo ni wa lazima ili kurejesha uimara wa goti lake na kumwezesha kurejea uwanjani akiwa imara.
Kwa mujibu wa ripoti ya kitabibu, nyota huyo kutoka Guinea atakuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki 8–10, hatua ambayo inamaanisha Simba italazimika kumkosa kwenye michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya CAF wakati akiendelea na tiba na mazoezi maalumu ya kurejesha utimamu wa mwili.
Lango la Simba kwa sasa litaendelea kuwa chini ya mlinda mlango wa Tanzania Yakoub Suleiman.
The post Camara kufanyiwa upasuaji wa goti kesho first appeared on SpotiLEO.







