PARIS: TIMU ya Taifa ya Ufaransa imeonesha tena ubora wake katika michezo ya kufuzu baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Ukraine, ushindi uliowahakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya nane mfululizo.
Nahodha wa kikosi hicho Kylian Mbappé aliibeba Les Bleus kwa kufunga mabao mawili kipindi cha pili katika mchezo uliobeba hisia nyingi, ukichezwa siku ya kumbukizi ya miaka 10 tangu mashambulizi ya Paris yaliyosababisha vifo vya watu 130.

Nahodha huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 58 kwa mkwaju wa penalti kabla ya Michael Olise kuongeza la pili dakika ya 76. Kisha Mbappé akarudi tena kufanya yake kwa bao la tatu, na Hugo Ekitike akahitimisha karamu hiyo ya mabao kwa la nne mwishoni mwa mchezo.
Ufaransa imefuzu ikiwa inaongoza Kundi D ikiwa na pointi 13 zilizotokana na mechi tano, ikiiacha Iceland iliyo nafasi ya pili kwa gepu la la pointi sita lisiloweza kufikiwa.
Kwa matokeo hayo, Les Bleus pia watakuwa miongoni mwa waliopangwa kwenye pot 1 katika droo ya fainali hizo zitakazofanyika Marekani, Mexico na Canada kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, droo ikifanyika Desemba 5.
Fainali za mwaka ujao zitakuwa za mwisho kwa kocha Didier Deschamps akiwa kwenye benchi la Ufaransa. Timu hiyo itamaliza mechi zake za kufuzu dhidi ya Azerbaijan Jumapili.

The post Mbili za Mbappé zaipeleka Ufaransa Kombe la Dunia first appeared on SpotiLEO.







