TASHKENT: TIMU ya Taifa ya Uzbekistan itashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwakani, na viongozi wao wanasema malengo yao ni kujenga timu na kupata uzoefu badala ya kutafuta mafanikio ya haraka.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Uzbekistan, Ravshan Irmato ambaye aliwahi kuchezesha mechi kwenye Kombe la Dunia mara tatu amesema kufuzu kwao ni hatua nyingine muhimu katika safari yao ya muda mrefu ya maendeleo.
Irmatov amesema kufuzu kwao ni ndoto ya watu milioni 38 waliyoisubiri kwa miaka 34 tangu nchi hiyo ipate uanachama wa FIFA mwaka 1994 baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti.
Alisisitiza kuwa kwa kuwa hii ni mara yao ya kwanza, haina maana kuweka malengo makubwa yatakayowatia presha wachezaji na kocha badala yake wanapaswa kutulia, kujipanga vizuri na kuruhusu matokeo yajitokeze.
Kwa mujibu wake, lengo lao kuu si ushindi mkubwa, bali kuendeleza soka lao kwa hatua za msingi hadi pale watakapoweza kuweka malengo ya juu kama mataifa makubwa ya soka.
Aliongeza kuwa ingawa Uzbekistan bado iko nyuma ya mataifa yaliyoendelea kisoka, kasi ya maendeleo kwa sasa ni kubwa, na anaamini mkakati mzuri wa maendeleo utawafikisha mbali.
Kufuzu kwao kumekuja baada ya majaribio saba tangu 1994. Licha ya kukaribia mara kadhaa, upanuzi wa Kombe la Dunia kutoka timu 32 hadi 48 pamoja na kazi ya ndani ya kukuza mchezo kumewezesha Wauzbeki kupata nafasi yao kwa utulivu katika michuano ya Marekani, Canada na Mexico.
The post Uzbekistan Kwenda kujifunza kombe la Dunia 2026 first appeared on SpotiLEO.




