CAIRO: VIGOGO wa Afrika, Al Ahly, Mamelodi Sundowns na Esperance de Tunis, Simba na Yanga wanatarajiwa kulinda heshima ya nyumbani katika mechi zao za ufunguzi wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) msimu wa 2025/26.
Bingwa wa kihistoria wa mara 12, Al Ahly ya Misri, wataingia kwenye Derby ya Afrika Kaskazini watakapovaana na JS Kabylie ya Algeria katika mchezo wa Kundi B utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Nchini Afrika Kusini, mabingwa watetezi wa PSL, Mamelodi Sundowns, watakuwa na kazi moja tu kushinda pale watakapowakaribisha FC Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo katika dimba la Loftus Versfeld jijini Pretoria, katika mechi ya Kundi C inayowakutanisha wakilishi wawili wa ukanda wa SADC.

Mjini Tunis, miamba ya soka la Tunisia, Esperance de Tunis, wataanza kampeni yao ya Kundi D wakitafuta ushindi wa nguvu dhidi ya mabingwa wa Mali, Stade Malien, kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi.
Hatua ya makundi inaanza kesho Ijumaa, ambapo Al Hilal Omdurman ya Sudan watakuwa wenyeji wa MC Alger ya Algeria katika mchezo wa Kundi C utakaopigwa kwenye uwanja wao wa muda, Amahoro Stadium, Kigali, Rwanda.
Jumamosi itashuhudia michezo sita, ikiwemo mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Pyramids FC ya Misri, wakianza kutetea taji lao kwa kuikaribisha Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa Kundi A utakaofanyika kwenye Uwanja wa 30 June jijini Cairo.

Ukanda wa Afrika Mashariki, mabingwa wa Tanzania, Young Africans (Yanga), watawakaribisha AS FAR Rabat ya Morocco katika Uwanja wa Amaan Zanzibar, katika pambano la Kundi B.
Wakati huohuo, mabingwa wa Morocco, RS Berkane, wataikabili Power Dynamos ya Zambia katika uwanja wa Berkane Municipal kwenye mechi ya Kundi A.
Mchezo wa mwisho wa wiki hii wa michuano hiyo utawakutanisha Simba SC ya Tanzania na Petro Atlético ya Angola katika mchezo wa Kundi D utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
The post Hapatoshi CAFCL wikiendi hii first appeared on SpotiLEO.





