BARCELONA: KOCHA Hansi Flick wa mabingwa watetezi wa LaLiga FC Barcelona amesema winga Lamine Yamal, aliyeikosa Hispania katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwezi huu kutokana na majeraha ya nyonga, yupo fiti kuelekea mchezo wa LaLiga dhidi ya Athletic Bilbao utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Camp Nou.
Yamal, ambaye amekosa mechi tatu msimu huu kwa matatizo ya nyonga tangu Septemba, anatarajiwa kurejea wakati Barcelona wakirudi nyumbani baada ya takribani miaka miwili na nusu, uwanja huo ukiwa umefunguliwa tena kwa uwezo mdogo kufuatia ukarabati unaoendelea.
“Amefanya mazoezi kwa bidii sana kwa wiki hizi mbili na ninafurahishwa sana na kile ninachokiona,” Flick amesema Ijumaa kuhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18, aliyerejeshwa kutoka kikosi cha Hispania Novemba 11.

Raphinha, ambaye amekuwa nje tangu Septemba kutokana na jeraha la misuli ya paja, naye yupo mbioni kurejea, lakini mshambuliaji Marcus Rashford ana shaka kuchezeshwa baada ya kupatwa na homa.
Kocha huyo amesema wachezaji wa Barcelona wanafurahia kurejea Camp Nou kwa mara ya kwanza tangu Mei 2023. Katika misimu miwili iliyopita, timu hiyo ilicheza mechi zake za nyumbani kwenye Uwanja wa Olimpiki, ambako Flick aliwaongoza kutwaa taji la ligi katika msimu wake wa kwanza, 2024/25.
“Nadhani tunapenda kucheza Camp Nou. Tulipokuwa mazoezini nilipopanda ngazi na kufika uwanjani ilikuwa hisia ya ajabu. Uwanja huu unaweza kutupa msukumo mkubwa sana kwenye mchezo, kwa sababu mashabiki wako karibu na wanafahamu kikamilifu timu inapohitaji msukumo huo” – Flick amesema.
Barcelona waliopo nafasi ya pili, wako nyuma ya Real Madrid kwa alama tatu kwenye LaLiga na wanashika nafasi ya 11 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo watakwenda kucheza na Chelsea Jumanne.

The post Raphinha, Yamal waamsha mzuka Barca first appeared on SpotiLEO.






