KIKOSI cha Yanga kimeondoka nchini jana kwenda Algeria kuwahi pambano la pili la Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikitoka kushinda dhidi ya AS FAR Rabat kwa bao 1-0, huku kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves akifichua siri inayombeba atangu ajiunge na timu hiyo Oktoba 15.
Ijumaa ya wiki hii ugenini Algeria, Yanga itavaana na JS Kabylie, ambayo ilianza vibaya kwa kufumuliwa mabao 4-1 na Al Ahly ya Misri, siku chache baada ya timu hiyo ya wananchi kupata ushindi kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar dhidi ya Far Rabat, shukrani kwa bao la Prince Dube.
Pambano la juzi lilikuwa la tatu kwa kocha Pedro kuiongoza Yanga tangu alipotua klabuni kuchukua nafasi ya Romain Folz aliyedumu kwa takribani siku 84 kutoka Julai 26, 2025 hadi Oktoba 18, 2025.
Katika mechi hizo tatu, Pedro ameiongoza Yanga kushinda zote zikiwamo mbili za Ligi Kuu Bara na moja Ligi ya Mabingwa na kocha huyo amesema siri ya mafanikio yake ni jinsi nyota wa kikosi hicho wanavyopambana sana kusaka ushindi ili kufikia malengo.
Pedro, raia wa Ureno, alikwenda mbali zaidi kwa kulichambua eneo la kiungo la timu hiyo akisema lina wachezaji wengi wanaompa wakati mzuri wa kuchagua kulingana na mpinzani wanayeenda kukutana naye.
“Katika eneo la kiungo, tunao wachezaji wengi, wote wakiwa na uwezo mkubwa na ushindani mkali. Hivyo ni jambo zuri kuwatumia ipasavyo,” alisema Pedro.
Hata hivyo, Pedro amebainisha katika eneo hilo kuna nyota ambao bado wanahitaji kuimarika ili kutoa ushindani zaidi jambo ambalo anaendelea kulifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi.
“Tuna wachezaji wanaofika wanane waliopo tayari kabisa kucheza eneo la kati. Naamini kila mechi huwa na mpango wake maalum na kila mchezo unahitaji sisi kujenga mkakati wa kuweza kuwashinda wapinzani wetu wote. Kwa hiyo naamini tumejenga njia hiyo vizuri na ninafurahia sana,” alisema Pedro na kuongeza;
“Pia nawapongeza wachezaji waliopata nafasi, ingawa baadhi yao bila shaka wanahitaji uzoefu zaidi, muda zaidi wa kucheza, na utulivu zaidi ili kushughulikia hali ya kushinda mechi dhidi ya wapinzani wakubwa. Kwa kucheza mara kwa mara, watapata uzoefu.
“Iwe tunashinda au la, lakini tunapata funzo la nini lingeweza kufanywa vizuri zaidi kwa siku zijazo. Kwa hiyo, tuko katika mchakato wa kujijenga tuwe bora zaidi na huo mchakato unatupa nguvu na kujiamini kwa wachezaji kuamini katika mawazo yetu na falsafa yetu.”
Katika mechi hizo tatu, Yanga imefunga mabao saba na kuruhusu moja ikianza kuichapa Mtibwa Sugar 2-0, ikailaza KMC kwa mabao 4-1 (zote katika Ligi Kuu) na wikiendi iliyopita AS FAR Rabat ikapigwa 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya Kundi B.
Katika eneo hilo la kiungo Yanga ina nyota kama Aziz Andabwile, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Shekhan Khamis, Moussa Balla Conte, Duke Abuya, Lasine Kouma na Mohamed Doumbia.
Nyota wengine wanaocheza eneo la kiungo wakitokea pembeni ni Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Offen Chikola na Edmund John ambao nao wamepata nafasi katika kikosi cha Pedro.
Katika mechi hizo tatu ambazo Pedro ameiongoza Yanga, Duke ndiye mchezaji pekee aliyeanza mechi zote eneo la kiungo cha kati, huku Mudathir akianza moja dhidi ya FAR Rabat baada ya awali kusumbuliwa na majeraha, hata hivyo, wakati wa kujiandaa na mechi hiyo, alikuwa bado hajawa fiti huku mwenyewe akifichua kwamba ilimlazimu kucheza kutokana na kuhitajika kufanya hivyo.
Mechi mbili za kwanza, Pedro pale kati alianza na Duke na Mohamed Doumbia ikiwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar na KMC, huku kiungo huyo raia wa Ivory Coast akiishia benchini Yanga ilipoichapa FAR Rabat.
The post BAADA YA KUANZA NA MGUU WA USHINDI ….MRENO ATAJA KINACHOMBEBA YANGA… appeared first on Soka La Bongo.


