DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Juma Mkambala ‘Jux’, amepokea kwa furaha mafanikio makubwa ya wimbo wake God Design baada ya kutambuliwa rasmi kuvuka streams zaidi ya milioni tano kwenye mtandao wa Spotify.
Wimbo huo ambao ameuachia kwa ushirikiano na mkali wa muziki kutoka Nigeria, Phyno, umeandika historia mpya ndani ya miezi sita pekee tangu kutolewa, hatua inayoonesha kasi ya ukuaji wa ushawishi wa Jux katika ramani ya muziki wa Afrika.
Tangu Mei 2025, God Design imeendelea kupenya kwenye playlists za mataifa mbalimbali na kujizolea mashabiki wapya kutokana na ubora wa sauti, ujumbe, na ladha ya kipekee ya R&B inayomtambulisha Jux katika anga la kimataifa.
Mafanikio haya yanaakisi uimara wa mashabiki wake, ubora wa utayarishaji chini ya Foxxmadeit, pamoja na nguvu ya brand yake ya Africanboy_hq ambayo imeendelea kupanuka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa sasa, God Design imeibuka kuwa wimbo wa Bongo Fleva uliotamba zaidi kwenye Spotify mwaka 2025, ikithibitisha kwa mara nyingine namna muziki wa Tanzania unavyozidi kuvuka mipaka na kufungua milango mipya ya kimataifa.
The post ‘God Design’ yapenya kimataifa kwa streams milioni 5 first appeared on SpotiLEO.



