MANCHESTER: KIUNGO wa Manchester city Tijjani Reijnders amesema hakuna sababu ya kupoteza kujiamini ndani ya klabu hiyo licha ya kichapo cha kushtua kutoka kwa Bayer Leverkusen kwenye Ligi ya Mabingwa ulaya usiku wa Jumanne.
Manchester City ilipoteza kwa mabao 2-0 nyumbani, mchezo ambao kocha Pep Guardiola aliamua kufanya mabadiliko 10 kwenye kikosi chake cha kwanza, hatua iliyosababisha kukatisha rekodi yao ya kutopoteza kwenye hatua ya ligi ya mashindano hayo.
Kichapo hicho kilikuja siku chache tu baada ya Man City kulala dhidi ya Newcastle kwenye Premier League, kuongeza shinikizo kuelekea mechi yao ijayo dhidi ya Real Madrid. Lakini Reijnders anasema timu haitatetereka kutokana na vipigo hivyo mfululizo, akisisitiza umuhimu wa kutazama mchezo ujao wa ligi dhidi ya Leeds kwa mtazamo chanya na wa ushindani.

“Bila shaka ni pigo, lakini hatupaswi kupoteza kujiamini,” alisema kiungo huyo.
Reijnders alisisitiza kuwa ubora wa kikosi unabaki kuwa mkubwa na kuwa ni juu yao kurejesha mwenendo mzuri: “Tunaijua uwezo wetu na tulichoonyesha kabla. Tusipanic, bado tuna nafasi nyingi msimu huu.”
Guardiola aliwapumzisha nyota wengi akiwemo Erling Haaland, Phil Foden na Gianluigi Donnarumma, huku Nico González pekee akiendelea kwenye kikosi kilichoanza dhidi ya Newcastle.
Lakini mabao kutoka kwa Alejandro Grimaldo na Patrik Schick yaliipa Leverkusen ushindi, na hata kuingia kwa Haaland akiwa na mabao 32 msimu huu hakukuweza kubadili matokeo.
Reijnders amesisitiza kuwa matokeo hayo hayataathiri maandalizi yao dhidi ya Real Madrid Desemba 10 katika uwanja wa Bernabéu.
“Siwazi kuwa kutakuwa na shinikizo zaidi, Tunajua tutakachokutana nacho Madrid, lakini bado kuna muda. Kwanza tujiandae kwa mchezo wa Jumamosi.” – amesema
The post “Bado tuko Imara” – Reijnders first appeared on SpotiLEO.







