LONDON: ILE vita iliyosubiriwa kwa hamu ya vijana barobaro Estevão na Lamine Yamal pale Stamford Bridge iliamuliwa kwa kishindo, baada ya Estevão wa Chelsea kung’ara na kufunga bao maridadi katika ushindi wa 3-0, huku Lamine Yamal wa Barcelona akiwa kimya sawa na wenzake wengi.
Estevão alikimbia kwa kasi akiwapita mabeki wawili kabla ya kupiga shuti kali lisilozuilika hadi juu ya nyavu kutoka ‘engo’ finyu na kuwapa Chelsea bao la pili dakika ya 55 kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa. Barcelona tayari walikuwa wamejifunga mapema, na Liam Delap akaongeza bao la tatu baadaye.
Katika kipindi cha kwanza kilichotawaliwa na Chelsea, Estevão alikuwa mwiba mkali akiichokonoa safu ulinzi wa Barcelona, japokuwa alipoteza nafasi kadhaa. Hata hivyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 alionesha kujiamini kwa kiwango cha juu, na baada ya bao lake, alilitaja kuwa tukio bora zaidi katika mwanzo wa safari yake ya soka.

“Sina maneno ya kutosha kuelezea hisia zangu. Yote yalitokea haraka sana, nikajipenyeza tu. Natumai kufunga mabao mengine mengi. Bila shaka hili ni tukio maalum zaidi kwenye maisha yangu ya soka. Nimefurahi familia yangu imekuwepo kunitazama.” – Mbrazil huyo amesema.
Kocha wa Chelsea Enzo Maresca alijaribu kupunguza presha na gumzo linalomzunguka nyota wake huyo mchanga, hata hivyo hakuficha kuvutiwa na ubora wa bao hilo.
“Ni ushindi mkubwa, hasa kwasababu ni dhidi ya Barcelona, lakini hakuna kilichobadilika kuhusu dhana ya timu yetu au malengo yetu. Estevão amecheza vizuri sana, si kwa sababu ya bao tu, bali pia kwa namna alivyotusaidia kwenye mashambulizi.” – amesema Maresca.
The post Estevão amgaragaza Yamal, Maresca amsifu first appeared on SpotiLEO.








