MANCHESTER: KOCHA mkuu wa Manchester City Pep Guardiola amejitwisha zigo la lawama kwa kipigo cha kushtukisha cha mabao 2-0 dhidi ya Bayer Leverkusen katika Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumanne, akisema uamuzi wake wa kubadili kikosi kizima lilikuwa kosa kubwa.
Guardiola alifanya mabadiliko 10 katika kikosi kilichocheza mchezo wa Premier League wa wikiendi iliyopita, waliopoteza 2-1 dhidi ya Newcastle United, na kuwaacha nje nyota muhimu akiwemo mshambuliaji Erling Haaland, aliyefunga mabao 14 kwenye ligi msimu huu.
Kocha huyo alikiri mara moja kuwa uamuzi huo ulikuwa mbaya kupitiliza. “Palikuwa na mabadiliko mengi sana,” ndiyo maneno yake ya kwanza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo.
“Ninaamini msimu ni mrefu, kuna mechi kila baada ya siku mbili au tatu, kila mtu anapaswa kuhusishwa. Lakini huenda ilikuwa ni kupita kiasi baada ya kuona matokeo. Ni mara ya kwanza katika maisha yangu kufanya jambo kama hilo, na lilikuwa baya mno. Nimetambua hilo.” Amesema Pep
Akitetea mantiki yake, Guardiola alielekeza lawama kwa ratiba ngumu inayojumuisha mechi za ndani na majukumu ya kimataifa, hasa kwa Haaland ambaye hubeba jukumu la kufunga mabao kwa klabu hiyo na timu yake ya taifa.
“Nilihisi tu, tumekuwa tukifanya mazoezi vizuri, wachezaji wana uchangamfu. Nikaona twende mechi ni ya Champions League na tupo nyumbani, tuko kwenye nafasi nzuri pia. Na kwa mechi zinazofuata tuna Fulham, Sunderland, Real Madrid ziko nyingi mfululizo. Huwezi kumchezesha Erling dakika 95 kila wakati”. – aliongeza.

“Baada ya mapumziko ya kimataifa, sasa ni siku tatu au nne tu hadi Machi, na hakuna binadamu anayeweza kuhimili kiwango hicho.”
Guardiola aliongeza kuwa wachezaji aliowaanzisha walionekana kucheza kwa tahadhari isivyo kawaida.
“Nadhani walikuwa wanacheza ili wasifanye makosa, wakiepuka kuumiza timu. Huwezi kucheza ukiwa huru na umetulia.”
Kipigo hicho kimesitisha rekodi ya Man City ya mechi 23 bila kupoteza nyumbani katika hatua ya makundi au ligi ya Champions League, na kuwaacha katika nafasi ya sita wakiwa
na pointi 10 baada ya mechi tano. Timu nane za juu baada ya mechi nane za hatua ya ligi zinafuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.
City watakutana na Real Madrid katika mechi yao ijayo ya Champions League Desemba 10, huku Guardiola akionekana kutokuwa na wasiwasi kuhusu nafasi yao katika kufuzu.
The post Guardiola ajitwisha zigo la lawama Man City first appeared on SpotiLEO.









