LONDON: KOCHA wa vinara wa ligi kuu ya England Arsenal Mikel Arteta amesema nahodha wa timu hiyo, Martin Ødegaard, ana nafasi ya kurejea uwanjani baada ya kupona jeraha kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich leo usiku.
Ødegaard amekuwa nje ya kikosi cha washika mitutu hao tangu Oktoba kutokana na jeraha la goti, lakini sasa yupo kwenye mazoezi na kikosi cha kwanza kabla ya Bayern kuitembelea Emirates Stadium.
Kuhusiana na uwepo wake kwenye kikosi cha kuanza, itakuwa ni msaada mkubwa kwa Arsenal wanapolenga kushinda mechi ya tano mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu.

“Alikuwa karibu kucheza mechi iliyopita, hivyo tunayo matumaini kuwa ataweza kuwa kwenye kikosi,” Arteta aliwaambia waandishi wa habari.
Arsenal na Bayern wameanza wiki hii wakiwa timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa, huku Gunners wakitafuta kupiga hatua zaidi kwenye safari yao ya kufuzu hatua ya 16 bora kwa kuwafunga mabingwa hao wa Ujerumani.
Kikosi cha Arteta kinaingia kwenye mchezo huu uliosubiriwa kwa hamu baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya mahasimu wao wa Kaskazini mwa jiji la London, Tottenham, kwenye Premier League Jumapili.
The post Ødegaard mguu sawa kuwavaa Bayern first appeared on SpotiLEO.








