NEWCASTLE: KLABU ya Newcastle United ya Ligi kuu ya England imeibua madai kuwa Mashabiki wake walishambuliwa na kunyanyaswa na polisi wa Ufaransa baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wa Jumanne usiku dhidi ya Marseille.
Newcastle imesema katika taarifa yake kuwa imetuma malalamiko rasmi kwa shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, polisi wa Ufaransa na klabu ya Marseille kutokana na kile ilichokitaja kuwa matendo yasiyokubalika dhidi ya mashabiki wake.
Katika mchezo huo ambao Marseille iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Velodrome. Newcastle imedai kuwa mashabiki wake walizuiliwa uwanjani hadi kwa takribani saa moja baada ya filimbi ya mwisho.
Waliruhusiwa kutoka makundi ya watu 500 huku polisi wakiwasindikiza hadi kituo cha treni (metro).
“Mara tu kundi la kwanza lilipoachiliwa, polisi walianza kutumia nguvu zisizohitajika na zisizo na uwiano ili kuwazuia mashabiki wengine kusogea mbele. Hatua hiyo ilihusisha matumizi ya pilipili (pepper spray), marungu na ngao, na mashabiki wengi walipigwa bila kujali” – Imesema taarifa ya Newcastle
Klabu hiyo imetoa wito kwa UEFA na Marseille kufanya uchunguzi wa kina, huku ikishirikiana na polisi wa Uingereza kukusanya ushahidi.
“Usalama na ustawi wa mashabiki unapaswa kuwa kipaumbele cha juu wakati wote, na tunalaani vikali namna mashabiki wetu walivyotendewa na polisi katika tukio hili,” – taarifa iliongeza.
The post Newcastle yalia na Polisi wa Ufaransa first appeared on SpotiLEO.



