OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Zubeda Sakuru, amesema klabu hiyo imepata mafanikio makubwa kwa msimu wa 2024-2025, licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza.
Akizungumzia katika mkutano mkuu wa mwaka wa Simba uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Zubeda amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Huwezi kulinganisha msimu wa 2024-2025 na 2023-2024, kiukweli kuna vitu vingi vya kimaendeleo ambao tumefikia kama klabu, hii ni kwa sababu moja tu ya umoja na mshikamano baina yetu,” amesema.
Aidha, Zubeda amesema takwimu za Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) zinazoifanya timu hiyo kushika nafasi ya tano ni kuonyesha jinsi gani viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki wa kikosi hicho wanaongozwa kwa umoja wa falsafa ya umoja na mshikamano uliopo.
Katika hatua nyingine, Zubeda, amesema klabu hiyo imeweka rekodi mpya ya mapato ya kukusanya zaidi ya Sh660 milioni katika tamasha la Simba Day lililofanyika msimu uliopita.
“Haya ni mafanikio makubwa kwa sababu haijawahi kutokea kwa miaka ya nyuma, naamini msimu huu pia ambao tunaenda kutimiza miaka 90, tunaweza kuweka rekodi nyingine mpya kwa sababu ya huu umoja wetu.”
Kuhusu Uwanja wa Bunju Mo Arena, Zubeda amesema tangu msimu uliopita hadi sasa timu hiyo imeokoa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kufanya mazoezi yaliyowapunguzia gharama za kukodi viwanja vingine.
“Dhamira kuu ni kuukarabati zaidi uwanja ule, ili ukidhi mahitaji yanayohitajika kwa sababu tunaona umekuwa ni msaada mkubwa kwetu kwa miaka ya mbeleni, kuanzia timu zetu zote za wakubwa, vijana na wanawake,” amesema.
Kuhusu changamoto za klabu hiyo kwa msimu uliopita, Zubeda amesema kuna maeneo makubwa ambayo kwa kweli hawajayatimiza, ingawa kuna mwelekeo mzuri unaohitaji subra.
“Klabu zote duniani zinapitia changamoto, ila tofauti yetu sisi na wengine ni umoja na mshikamano uliopo, ambao siku zote umekuwa ndio nguzo muhimu ya kutuongoza.”
The post CEO ….MAFANIKO YETU MSIMU ULIOPITA NI KUKUSANYA MIL 600 SIMBA DAY NA KUSHIKA NAFASI YA PILI… appeared first on Soka La Bongo.



