DAR ES SALAAM: BAADA ya pilikapilika za mashindano ya kimataifa, vigogo wa soka nchini Simba, Azam FC na Singida Black Stars wanarejea kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakitafuta kuondoa machungu ya matokeo mabaya kwenye michuano ya CAF.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho kutwa kuivaa Mbeya City, ikitokea kwenye kupoteza michezo miwili mfululizo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Wekundu wa Msimbazi walipoteza kwa mabao 1-0 dhidi ya Petro Atletico na Stade Malien.
Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kusahau matokeo hayo na kuelekeza nguvu kwenye kurejea kwenye ligi kwa ubora.
Amesema timu imejipanga upya na itafanya maboresho katika dirisha dogo kabla ya kuvaana na Esperance, mechi inayotarajiwa kupigwa kabla ya Sikukuu ya Krismasi.
Kwa upande wa Azam FC, nao wanarudi kusaka utulivu baada ya kupoteza michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika—wakifungwa 1-0 na Wydad pamoja na 2-0 dhidi ya Maniema Union ya DR Congo. Wanalazimika kuweka pembeni maumivu ya kimataifa na kujiandaa upya kwa mchezo wao wa ligi dhidi ya Singida Black Stars.
Singida nao hawaji kwa wepesi, kwani wametoka kwenye michuano ya CAF wakipata sare moja na kupoteza mchezo mmoja, hali inayowafanya pia kuhitaji pointi muhimu kurejesha morali ya kikosi.
Kwa ujumla, michezo yote ya wiki hii haitarajiwi kuwa rahisi. Timu zinazokutana zinakuja na kiu ya kupata matokeo chanya baada ya misimu tofauti ya kimataifa. Kila mmoja anahitaji pointi tatu za kurejesha imani kwa mashabiki na kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.
Huenda vigogo hawa wakarejea kwa kasi na hamasa mpya, wakitumia michezo ya ligi kama dawa ya kufuta machungu ya safari zao za Afrika.
The post Simba, Azam vita yarudi upya Ligi Kuu first appeared on SpotiLEO.






