LONDON: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, ametoa wito wa nguvu na msisimko mkubwa kwa wachezaji wake na mashabiki wakati kikosi chake kikijiandaa kuvaana na Brentford leo Jumatano, mchezo muhimu baada ya sare mbili katika mechi tatu za Premier League zilizopunguza kasi yao.
Arsenal, wanaoongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili na mchezo mmoja mkononi, wanaendelea kusaka taji lao la kwanza tangu 2004 baada ya kumaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo. Na Arteta amesisitiza kuwa mechi hiyo ni nafasi ya kurejesha kasi yao.
“Ni fursa nyingine saa 1:30 jioni (saa za England) kila mtu anapaswa kuwa Emirates, kushangilia na kutuhamasisha kushinda mchezo. Tuwe kama Wanyama tupige kelele tushangilie tupambane kumfunga Brentford ni fursa kubwa na muhimu sana” – Arteta amewaambia waandishi wa habari.
Hata hivyo, Arsenal inaweza kukumbana na kukosekana kwa wachezaji muhimu. Beki William Saliba na winga Leandro Trossard wana hatihati ya kucheza baada ya kukosa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Chelsea Jumapili kutokana na majeraha. Beki Gabriel na mshambuliaji Kai Havertz bado wana wiki kadhaa za kuendelea kupona.
“Wachezaji hawafanyi mazoezi katika nafasi fulani kisha kulazimika kucheza nafasi hiyo, msimu huu umekuwa mbaya zaidi katika maeneo kadhaa kikosini, hasa safu ya ushambuliaji, na sasa kinachotokea kwenye safu ya ulinzi,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kikosi cha Arsenal sasa kimejengeka vyema na kuwa bora zaidi kutokana na uzoefu walioupata misimu iliyopita.
“Tumejifunza na tumetengeneza kikosi cha kutumainiwa zaidi na chaguzi nyingi. Tumejifunza pia kwamba tunapaswa kutumia wachezaji katika nafasi tofauti yofauti ili kushindana kwa kiwango hiki,” Arteta aliongeza.
The post Arteta awataka wachezaji, mashabiki kuwa kama ‘wanyama’ first appeared on SpotiLEO.






