LONDON: MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 100 ya Premier League kwa haraka zaidi, akifanya hivyo kwa kishindo katika mchezo wake wa 111 walipoibuka na ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Fulham, Jumanne usiku.
Haaland, mwenye umri wa miaka 25, alifunga bao hilo dakika ya 17 baada ya kupokea krosi ya Jeremy Doku na kumalizia kwa shuti kali la mguu wa kushoto. Ametimiza rekodi hiyo katika mechi 111, mechi 13 chini ya aliyekuwa mmiliki wa rekodi hiyo, Alan Shearer.
Ingawa Shearer bado anaongoza orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa EPL kwa mabao 260, kasi na uthabiti wa Haaland unaashiria safari yenye uwezekano mkubwa wa kuvunja rekodi hiyo siku za usoni.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola, hakuficha furaha yake.
“Kama ningeniambiwa atafunga mabao 100 katika mechi 111, ningejibu ‘Una uhakika?’ Hizi namba ni za ajabu. Ni kitu cha kushangaza. Alikuwa bora sana. Alifunga bao la kuvutia. Natumai ataendelea kuwa na njaa ya kufunga zaidi kwa klabu hii.” – amesema Guardiola.
Baba yake, Alf-Inge Haaland, alishuhudia tukio hilo kutoka jukwaani katika uwanja wa Craven Cottage, jambo lililoongeza uzito wa mafanikio hayo. Haaland pia alikiri umuhimu wa rekodi aliyoweka.
“Ni wakati wa kujivunia. Kuwa kwenye ‘The 100 club’ ni kitu kikubwa. Kufanya hivi haraka namna hii ni jambo la ajabu. Najiona mwenye furaha. Kama nilivyosema mara nyingi, kazi yangu kama mshambuliaji wa Manchester City ni kufunga mabao. Nilipaswa kuwa na hat-trick, nimekosa nafasi kadhaa. Nitafanya mazoezi zaidi.” – Amesema Haaland
Akiwa kinara wa mabao msimu huu kwa mabao 15, Haaland aliganda kwenye mabao 99 kwa mechi mbili mfululizo baada ya kukosa nafasi dhidi ya Newcastle na Leeds. Kwa Man City ambao bado wanasaka mataji msimu huu, njaa ya mabao ya Haaland inaonekana kuongezeka badala ya kupungua.
The post Haaland aweka rekodi mpya EPL first appeared on SpotiLEO.






